Migogoro ya kisiasa na hatima ya demokrasia

Thursday December 09 2021
MIKAKATIPIC
By Peter Elias

Migogoro ndani ya vyama vya siasa imekuwa ni maisha ya kila siku kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo.

Licha ya migogoro hiyo kuathiri ukuaji wa vyama husika, lakini bado utatuzi wake si wa kasi kama inavyotarajiwa na wadau wa kisiasa ambao wanapenda kuona uimara wa vyama.

Tangu mfumo wa vyama vingi urejee hapa nchini mwaka 1992 na kushuhudiwa uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama vingine mwaka 1995, vyama vya upinzani ndivyo vimeonekana kuathirika zaidi tofauti na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Maelewano hafifu kati ya viongozi na viongozi, viongozi na wanachama, makundi yanayozuka nyakati za uchaguzi wa ndani, matumizi na mgawanyo wa fedha ni miongoni mwa sababu za migogoro hiyo ambayo imeua na kuzorotesha baadhi ya vyama.

Ujio wa vyama vingi ulitabiriwa kukuza demokrasia na kutanua wigo wa watu kuchagua na kuchaguliwa, lakini kadri siku zinavyokwenda ndivyo matarajio husika yanavyodidimia.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Andrew Bomani anasema vyama vya siasa nchini havina demokrasia kwa sababu vinaongozwa kwa matakwa ya Mwenyekiti na akitokea mwanachama akahoji na kupinga baadhi ya mambo anaonekana msaliti.

Advertisement

Bomani anapendekeza kwamba viongozi wa vyama vya siasa nao wapatiwe mafunzo maalumu ya uongozi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na kuepusha migogoro inayotokea ndani ya vyama hivyo.

“Pendekezo langu ni kwamba viongozi wa vyama vya siasa wapatiwe mafunzo pale NDC ili wawe na uwezo wa kushughulikia migogoro badala ya kuwa chanzo,” anasema Bomani.

Anasema kutokana na kushamiri kwa migogoro, anapendekeza kuwe na chombo kingine maalumu mbali na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambacho kitakuwa na jukumu la kusikiliza migogoro kwenye vyama vya siasa na kuipatia ufumbuzi.

“Kitafutwe chombo kingine cha kutatua migogoro ya kisiasa ambacho kitaaminika na kila chama,” anasema Bomani.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Awadh Mustapha anasema migogoro ndani ya vyama vya siasa inatokea kwenye masuala ya uongozi na fedha, hivyo ni muhimu kwa vyama kutambua nafasi yao na kuweka utaratibu mzuri.

“Viongozi waache tamaa na uchu wa madaraka, watoe nafasi kwa makada wengi waongoze ili kuleta mabadiliko chanya kwenye vyama husika”.

Anakiri kwamba kuna umuhimu wa viongozi hao kupata mafunzo iwe katika chuo cha NDC au Taasisi ya Uongozi ili kuwajengea uwezo wanasiasa nao kuyakabili majukumu ndani ya vyama vyao na kuvisaidia kustawi zaidi.

“Kwa kweli mafunzo kwa wanasiasa ni muhimu, tuna taasisi nyingi zinazotoa mafunzo hayo, ni vizuri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikaratibu suala hili kuwasaidia viongozi hawa,” anasema Mustapha.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Frank Kimaro anasema elimu ni muhimu kwa mtu yoyote, hata wanasiasa wanahitaji mafunzo ili wakipata dhamana ya kuongoza nchi basi wawe na ujuzi.

“Vyama vya siasa vinalea viongozi ambao wakipewa dhamana wanakwenda kusimamia rasilimali katika nchi hii, kwa hiyo ni vizuri wakapatiwa mafunzo ya uongozi kama ilivyo kwa viongozi wengine,” anasema.

Mwanazuoni huyo anasema vyama vya siasa ni taasisi za umma, hivyo viongozi wa vyama vya siasa nao wachukuliwe kwa umuhimu wao ili nao wawe na maarifa ya kuvijenga vyama vyao na kuweza kushindana kwenye chaguzi.

Chama cha Wananchi (CUF) ni miongoni mwa vyama vya upinzani vilivyojizolea umaarufu mkubwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini, lakini nacho kimekumbwa na dhoruba la migogoro na kukifanya kidhoofike.

Licha ya mara kwa mara kuchukua hatua za kudhibiti wanaosababisha migogoro husika, ikiwamo kuwaonya na kuwafukuza baadhi ya makada, bado kimeshindwa kuimarika.

CUF kimekuwa kikiandamwa na migogoro mingi kwa nyakati tofauti na kuna wakati walilazimika kuwavua uanachama viongozi wa juu, akiwamo Katibu Mkuu.

Mkutano Mkuu wa CUF wa Machi 14, 2019 uliamua kumvua uanachama aliyekuwa Katibu Mkuu, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye baada ya azimio hilo alikimbilia Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Machi 18, 2019, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ilikubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF, licha ya kujiuzulu wadhifa huo mwaka 2015.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ulimaanisha kwamba Maalim Seif Sharif Hamad si Katibu Mkuu wa CUF kwa hatua ambazo upande wa Profesa Lipumba iliuchukua kwa kumchagua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa Katibu Mkuu.

Hukumu ya kesi hiyo ilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho (baadhi ya wajumbe wanaomuunga mkono Maalim Seif), dhidi ya Profesa Lipumba na msajili wa vyama wakipinga uamuzi wa msajili kumtambua Profesa Lipumba kuwa bado ni Mwenyekiti halali wa CUF.

Mbali na Maalim Seif, wengine waliotimuliwa uanachama kwenye mkutano huo ni Ismail Jussa, Salim Bimani, Issa Kheri, Mohammed Nuru na Said Ali Mbarouk (kutoka Zanzibar) na Joran Bashange, Mbarara Maharagande na Abdallah Katawi (Tanzania Bara) kwa madai ya kushabikia na kuongeza kesi za CUF.

Novemba 9, 2021 Baraza la Uongozi la CUF liliazimia kwa kauli moja kumvua uanachama aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya kwa tuhuma za kula njama na kukihujumu chama.

Mbali na Kambaya, wengine waliofukuzwa ni aliyekuwa mgombea mwenza wa Profesa Ibrahimu Lipumba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Hamida Abdallah Huweishi na Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (JUVICUF), Chande Jidawi.

Wengine ni Ali Makame Issa, Mtumwa Ambari Abdallah, Mohamed Vuai Makame na Dhifaa Bakari ambao wote ni wajumbe wa Baraza Kuu la CUF.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya vijana wa chama cha Cuf (Juvicuf), Iddi Mkanza anasema Juvicuf inaunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi wa kuwavua uanachama makada kwa madai kwamba wamevunja katiba ya chama kwa kula njama na kutoheshimu viongozi wake.

Migogoro ya kisiasa haipo ndani ya CUF pekee, bali mwaka 2013 Chadema kiliwavua uongozi wanachama wake watatu, Zitto Kabwe, Profesa Kitila Mkumbo (Waziri Viwanda na Biashara), Samsom Mwigamba ambao wanadaiwa waliandaa waraka wa kuupindua uongozi uliokuwa chini ya Freeman Mbowe.

Zitto alikuwa kwenye mtafaruku mkubwa ndani ya chama hicho tangu alipotangaza kuwania uenyekiti akikabiliana na Mbowe mwaka 2009, hatua iliyoonekana kukigawa chama kwenye makundi mawili yaliyokuwa yakiwaunga mkono wanasiasa hao wawili.

Hali ilipozidi kuwa tete na Zitto kubanwa na wazee wa chama hicho waliozungumza naye mwishoni aliamua kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Februari 28, 2020 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alifukuzwa uanachama CCM kwa kwenda kinyume cha utaratibu wa chama hicho, ingawa mwenyewe alisema sababu kubwa ya uamuzi huo ni kutokana na dhamira yake ya kumkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, hayati John Magufuli katika kuwania urais wa 2020.

Desemba 4, 2019 Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye akiwa ni miaka minne tangu ajiunge na upinzani akitokea CCM aliamua kujiondoa Chadema baada ya kushindwa kutetea Uenyekiti wa Kanda ya Pwani.

NCCR-Mageuzi haikusalimika na upepo huu mbaya, kwani baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 kiliingia kwenye mtafaruku wa uongozi uliozaa makundi mawili, moja likimuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Agustine Mrema dhidi ya Katibu Mkuu Mabere Marando.

Advertisement