Migogoro ya wazazi yatajwa kikwazo wanafunzi kufaulu
Chunya. Migogoro ya wazazi, ukatili wa kijinsia vimetajwa kuwa ni vikwazo kwa wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika masomo na kusababisha kuathirika kisaikolojia.
Kufuatia hali hiyo uongozi wa Shule ya Holyland mchepuo wa kiingereza ,umeweka utaratibu wa kutumia wataalamu wa saikolojia kuzungumza na wanafunzi wanaporejea kutoka likizo.
Mkurugenzi wa Shule hiyo, Lawena Nsonda ameiambia Mwananchi Digital na kukiri kuwapo kwa changamoto hizo kwa baadhi ya wanafunzi wanabainika na wanashauriwa na kurejea katika hali ya kawaida na kufanya vizuri kwenye masomo huku sababu kubwa ni ukatili wa kuathiri akili kufuatia kushuhudia migogoro ya wazazi na walezi.
“Awali ilikuwa ikitupa shida kujua sababu za baadhi ya wanafunzi kutofanya vizuri katika masomo licha ya jitihada za walimu, lakini tulipoanza kutumia wataalamu wa saikolojia tukabaini kuna changamoto sana watoto wanaporejea kwenye familia wakati wa likizo kufuatilia migogoro ya wazazi, ”amesema.
Nsonda amesema baada ya kubaini changamoto hiyo ameweka mikakati mitano ikiwepo kuzungumza na wazazi,kutoa elimu ya saikolojia kwa watoto waliathirika ,kufunga mifumo ya kamera kufuatilia mienendo ya wanafunzi wa bweni, walimu na watumishi sambamba na milo mitano kwa siku hususan kwa watoto wa darasa la nne.
Kwa upande wake, Ezekiel George Mwalimu wa kiroho na mtaalam aa saikolojia ,amesema jambo kubwa katika kuzungumza na kundi hilo pia ni kumtanguliza Mungu sambamba na kuzungumza na wanafunzi wenyewe ambao tunawabaini kwa kufanya nao mazungumzo.
“Tunawabaini wanafunzi kwa kuwapima uelewa,uvuvi,muda mwingi kuwa mnyonge na hata kutochangamka na ndio nakaa nao,nae kumuhoji mwisho wa siku ana eleza kile kinachomsibu huku asilimia kubwa imekuwa ni migogoro ya wazazi”amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amepongeza utaratibu wa Shule hiyo kutumia wanasaikolojia kuzungumza na wanafunzi jambo hilo litasaidia kuwa na kizazi bora.
“Mkoa wa Mbeya ni miongini mwa mikoa ambayo imekithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto walio na umri wa miaka 0-18 jambo ambalo linamlazimu kutenga muda kupita katika Shule za msingi, Sekondari ,vyuoni kutoa elimu ”amesema.
Ametaja changamoto inayochangia ni migogoro ya kifamilia katika ndoa ambayo inachangia watoto kuathirika kisaikolojia kuacha masomo na kukimbilia mitaani na huku akipongeza hatua ya uongozi wa shule hiyo kuisaidia Serikali kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto.