Prime
Mihogo ya kuchoma ilivyosababisha mtoto kumuua mama yake
Muktasari:
- Kulingana na hati ya mashitaka, ilidaiwa mchana wa Oktoba mosi, 2024 katika Kijiji cha Mpalahala ndani ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, mshtakiwa alimuua mama yake Fatuma Omary Abdallah au Fatuma Omary Samanjonge.
Korogwe. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Tanga iliyoketi Korogwe, imemtia hatiani Said Seif Mnaguzi kwa mauaji ya kukusudia ya mama yake mzazi, huku kiini cha mauaji kikitajwa ni hatua ya mama kuondoa mihogo aliyokuwa akiichoma.
Hata hivyo, ingawa ripoti ya uchunguzi wa kitabibu wa akili ya mshitakiwa imethibitisha hakuwa na tatizo la afya ya akili wakati akifanya mauaji hayo, katika usikilizwaji wa shauri hilo alionesha mwenendo wa uwendawazimu.
Mshtakiwa aliendelea kuonesha tabia iliyoashiria kuwa na uelewa hafifu wa mwenendo wa kesi hiyo na badala ya kujibu masuala yanayohusiana na shtaka, mara kwa mara alizungumzia mambo yasiyohusika, ikiwamo mechi za soka.
Katika hukumu yake, Jaji Happiness Ndesamburo amesema kuna wakati mshitakiwa alitoa kauli zinazokinzana, ikiwamo kukiri kumuua marehemu, kauli iliyoonekana pia wakati wa usikilizaji wa utetezi.
“Kwa kukosekana kwa ushahidi wowote wa kimatibabu unaoonesha mshtakiwa alikuwa na tatizo la akili wakati wa kutenda kosa hilo, kwa kuzingatia ripoti ya daktari wa magonjwa ya akili inayothibitisha alikuwa na akili timamu wakati huo, Mahakama hii imeridhika mshtakiwa alitenda kosa aliloshtakiwa nalo,” amesema Jaji Ndesamburo katika hukumu yake.
Hata hivyo, Jaji Ndesamburo amesema kwa kuzingatia mwenendo wake katika kipindi chote cha kesi, Mahakama inaona kuwa hii ni kesi inayofaa kutumika kwa kifungu cha 237(1)(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
“Baada ya kumtia hatiani mshtakiwa, kwa kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, naagiza azuiwe kwa muda utakaoamuliwa na Rais na kushughulikiwa kwa mujibu wa vifungu vya 237(2) na (3) vya CPA,”amesema Jaji Ndesamburo.
Chini ya vifungu 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia huhukumiwa adhabu ya kifo lakini hali inakuwa tofauti endapo mtu huyo anaonekana kuwa na matatizo ya akili wakati wa kesi yake.
Tukio la mauaji lilivyotokea
Kulingana na hati ya mashitaka, ilidaiwa mchana wa Oktoba mosi, 2024 katika Kijiji cha Mpalahala ndani ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, mshtakiwa alimuua mama yake Fatuma Omary Abdallah au Fatuma Omary Samanjonge.
Siku hiyo saa sita mchana, marehemu alikuwa nyumbani kwake Kijiji cha Mpalahala pamoja na watoto wake, akiwamo shahidi namba moja wa upande wa mashitaka, Saumu Seif Mnaguzi na wanafamilia wengine pia walikuwapo.
Wakati huo walikuwa wakiishi katika nyumba moja, hivyo mshitakiwa alikuwa ameweka mihogo kwenye moto jikoni.
Fatuma alipoingia jikoni akikusudia kuandaa chakula cha mchana, aliondoa mihogo kutoka kwenye moto.
Baadaye mshtakiwa alirudi na kuuliza ni nani aliyechukua mihogo yake, Fatuma alimweleza alifanya hivyo ili kuandaa chakula kwa ajili ya familia, mshtakiwa akakasirika sana, akamtukana na baadaye kumshushia kipigo mama yake.
Shahidi wa kwanza (Saumu), alitoa ushahidi kwamba baada ya kusikia ugomvi, alienda jikoni na kushuhudia mshtakiwa akimpiga Fatuma kichwani kwa kutumia fimbo, mara moja alikimbia kutafuta msaada kutoka kwa majirani.
Akiwa njiani, alikutana na shahidi namba mbili, Happy Dihawi, ambaye walirudi naye hadi nyumbani kwa Fatuma na walipofika,
Happy alisema walimkuta mshitakiwa akimshambulia Fatuma maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Shahidi huyo namba mbili wa mashitaka, alitoa ushahidi kwamba mshtakiwa alipomwona, alimsukuma marehemu kwa nguvu kuelekea ukutani na kumfanya aanguke chini, kisha akakimbia kutoka eneo hilo na kutokomea kusikojulikana.
Happy katika ushahidi wake amesema baada ya mtuhumiwa kukimbia, alimkagua Fatuma na kuona alikuwa amejeruhiwa sehemu ya nyuma ya kichwa na alikuwa akivuja damu hivyo aliamua kumtoa nje ya jiko.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, Fatuma hakuwa na mwitikio wa kutosha na alikuwa akipata shida kupumua na muda mfupi baadaye, wanakijiji wengine waliwasili, akiwamo Mohamed Omary Suleiman ambaye alikuwa shahidi namba tatu wa Jamhuri, ambaye wakati huo alikuwa Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mpalahala.
Shahidi huyo alimkuta Fatuma akiwa amelala nje ya nyumba yake huku akiwa na maumivu makali, akiwa na jeraha nyuma ya kichwa na damu ikimtoka puani na hapo alitoa maelekezo apelekwe Zahanati ya Kwediboma kwa ajili ya matibabu.
Akiwa hapo, alijulishwa kuwa mshitakiwa ndiye aliyefanya ukatili huo, hivyo aliwahamasisha wanakijiji, wakamtafuta mtuhumiwa na hatimaye wakampata katika Kitongoji cha Manga, alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi cha Kwediboma.
Ushahidi wa upande wa mashtaka ulieleza zaidi kuwa marehemu alipata matibabu ya awali katika Zahanati ya Kwediboma kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Handeni, alipofariki dunia jioni ya siku hiyo hiyo.
Utetezi wake ulivyokuwa
Baada ya kutakiwa kujitetea, mshtakiwa alitoa ushahidi chini ya kiapo na kukanusha shtaka la mauaji ya mama yake mzazi (Fatuma) alilokuwa ameshitakiwa nalo.
Alieleza siku hiyo ya tukio, alipokuwa akitoka saluni, alisimamishwa na dereva wa bodaboda anayeitwa Mondinga na kupelekwa moja kwa moja kituo cha polisi, hivyo hakuwahi kufika nyumbani wala kumshambulia marehemu.
Alikanusha kumuua mama yake na kudai mashahidi wa upande wa mashtaka walimhusisha na tukio hilo kwa uongo.
Wakati wa hatua zote mbili za kuongozwa kutoa ushahidi (examination in chief) na kuhojiwa na upande wa mashtaka (cross examination), mshtakiwa wakati mwingine alitoa majibu yasiyo na mantiki wala uhusiano na maswali yaliyoulizwa.
Hukumu ya Jaji Ndesamburo
Katika hukumu yake aliyoitoa Julai 2, 2026 na kuwekwa katika tovuti ya Tanzlii ya Serikali, Julai 6, 2026, Jaji Ndesamburo alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande mbili, ni wajibu wa kutafuta nani alifanya mauaji hayo.
Kwa kuanzia, Jaji alisema kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka, hakuna ubishi kuwa Fatuma kwa sasa ni marehemu na kwamba kifo chake kilikuwa si cha asili, bali kilikuwa na mkono wa mtu.
“Ushahidi wa shahidi namba nne wa upande wa mashtaka, ambaye alifanya uchunguzi wa maiti ya marehemu, ulikuwa wazi,”alisema Jaji.
“Alitoa ushahidi kwamba, wakati wa uchunguzi, mwili wa marehemu ulikutwa na uvimbe nyuma ya kichwa (kisogoni) uliotokana na mkusanyiko wa damu (haematoma), na kwa mujibu wa maoni yake ya kitaalamu, jeraha hilo liliashiria madhara yaliyosababishwa na kitu kizito chenye ncha butu.”
“Kwa kukosekana kwa dalili zozote za sababu za asili au uhalalisho wa kisheria, na baada ya kuzingatia kwa kina matokeo ya uchunguzi wa kimatibabu pamoja na mazingira yanayohusika, Mahakama hii inaamua na kushikilia kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kitendo kisicho halali na cha kikatili,”alieleza Jaji.
Katika kuthibitisha ni nani alihusika na kifo hicho, upande wa mashitaka uliegemea zaidi ushahidi wa shahidi namba moja na mbili ambao walishuhudia mshitakiwa akimshambulia Fatuma na walimtambua kikamilifu kwa kuwa ilikuwa mchana.
“Katika uchambuzi wa mwisho, naona kwamba utetezi uliotolewa na mshtakiwa hauondoi wala kutia shaka yoyote ya msingi kuhusu ushahidi thabiti na wa kuaminika wa utambuzi uliotolewa na shahidi namba 1 na 2,”alisema Jaji.
“Kwa hivyo, utetezi wa kutokuwa na nia mbaya unakataliwa. Kwa hivyo, ninahitimisha kwamb, upande wa mashtaka umethibitisha bila shaka yoyote kwamba ni mshtakiwa aliyesababisha majeraha mabaya kwa marehemu.”
“Ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukukanushwa katika vipengele vyote muhimu na haukudhoofishwa na utetezi wowote wenye mashiko,” alieleza.
“Hivyo basi, ninamtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Adhabu, na ninamhukumu hivyo.”
“Ingawa upande wa mashtaka umethibitisha kesi na Mahakama hii imebaini mshtakiwa alisababisha kifo cha marehemu kinyume cha sheria na kwa nia ovu iliyokusudiwa, mazingira ya kesi hii yanaitaka Mahakama kuzingatia hali ya akili ya mshtakiwa na athari yake katika uamuzi unaofaa kutolewa,” alisema Jaji.
“Katika kipindi chote cha mwenendo wa kesi, mshtakiwa alionesha tabia isiyo ya kawaida iliyozua wasiwasi kuhusu hali yake ya afya ya akili,” alieleza.
“Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, Mahakama ilibaini mara kwa mara alionekana kutofuatilia kinachoendelea, alitazama bila mwelekeo kwa muda mrefu, alionesha miondoko ya uvivu na, katika matukio kadhaa, alionekana kusinzia, hali iliyohitaji wakili wake au mhudumu wa Mahakama kumwamsha.”
Hivyo basi, kwa mujibu wa vifungu vya 219 na 220 vya CPA, Mahakama hiyo iliamuru mshtakiwa afanyiwe uchunguzi wa afya ya akili na majibu yalionesha alipofanya mauaji hayo alikuwa na akili timamu hivyo kesi kuendelea.