Miili ya mwalimu, mwanafunzi waliouawa Chunya yasafirishwa kwa maziko Iringa, Mbozi

Mwalimu Herieth Lupembe.
Muktasari:
Awali ilielezwa mwili wa mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Isenyela, Tatizo Haonga (16) ungezikwa Chunya
Mbeya. Miili ya mwalimu na mwanafunzi waliouawa na watu wasiojulikana wilayani Chunya mkoani Mbeya imeagwa, waombolezaji wakilaani mauaji hayo.
Waombolezaji wengi wamejitokeza katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki, Kigango cha Kiwanja leo Jumanne Aprili 2, 2024.
Akiongoza ibada, Padri wa kanisa hilo, Kazimoto amesema mwalimu Herieth Lupembe (37), alikuwa na mapenzi mema ya kumlea mtoto Tatizo Haonga (15), ambaye naye aliuawa.
Amesema alimfundisha maadili ya kimwili na kiroho.
“Marehemu (Tatizo) alikuwa akisali kwenye kanisa hili, Jumatatu ya Pasaka ilipaswa kuwa siku yake ya ubatizo lakini kwa bahati mbaya tumepokea tukio hilo baya mbele za Mungu,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiwanja, Gideon Kinyamagoha, amesema Serikali imeshiriki msiba huo sambamba na kutoa magari mawili kwa ajili ya kusafirisha miili ya marehemu na familia zao kwenda kuwasitiri katika mikoa ya lringa na Songwe. Pia imenunua majeneza.
Amesema Serikali imetoa basi kwa ajili ya kuwasafirisha wananchi kwenda mkoani Iringa kushiriki mazishi ya mwalimu Herieth.
“Wananchi wamechangia pesa ya mafuta ambayo yatatumika kwenda mkoani Iringa na kurejea baada ya kusikindikiza mwili wa Herieth,” amesema.
Mkazi wa Kiwanja, Joseph Mwailima amesema tukio hilo limewapa simanzi kutokana na namna walivyoishi na mwalimu huyo na kushirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Diwani wa Kata ya Mbugani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri, Bosco Mwanginde amesema wamepata pigo la kuondokewa na mwalimu huyo, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa na umri mdogo na bado alikuwa na mchango mkubwa kwa Taifa.
“Kimsingi imetusikitisha sana kikubwa tuendelee kukemea vitendo viovu na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi zinapojitokeza changamoto mbalimbali za uvunjifu wa amani,” amesema.
Herieth atazikwa mtaa wa Frelimo, Manispaa ya Iringa, huku Tatizo mwili wake umesafirishwa kwa maziko katika Kijiji cha Ihanda wilayani Mbozi, mkoani Songwe.
Awali, ilielezwa mwili wa Tatizo ungezikwa Kijiji cha Mbugani wilayani Chunya.
Machi 31, 2024 miili ya Herieth, aliyekuwa akifundisha Shule ya Msingi Mbugani na wa Tatizo, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Isenyela aliyekuwa akiishi naye ilikutwa ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi kwa kupigwa na vitu vyenye ncha kali.
Katika tukio hilo, Heris Barnabas (5), mtoto wa Herieth alijeruhiwa na amelazwa katika Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu.