Miili ya wanahabari yawasili uwanja wa Nyamagana

🔴#LIVE: Miili ya wanahabari watano na dereva ikiagwa

Muktasari:

Miili ya wanahabari na dereva wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza waliofariki katika ajali ya gari jana Januari 11 imewasili katika uwanja wa michezo wa Nyamagana tayari kwa ajili ya heshima za mwisho.

Mwanza. Miili ya wanahabari na dereva wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza waliofariki katika ajali ya gari jana Januari 11 imewasili katika uwanja wa michezo wa Nyamagana tayari kwa ajili ya heshima za mwisho.

Msafara wa magari yaliyobeba miili hiyo imewasili uwanjani asubuhi na kuzunguka uwanja kabla majeneza yaliyobeba miili ya marehemu kushushwa na maaskari wa vikodi vya ukinzi na usalama na kuwekwa eneo maalum iliyoandaliwa.

Jeneza lenye mwili wa Ofisa Habari mkoa wa Mwanza, Abel Ngaprmba ndio ulikuwa wa kwanza kushushwa kwenye gari na kuibua vilio miongoni mwa waombolezaji, hasa waandishi wa habari na wana familia.

Baada ya jeneza la Ngapemba, jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Ofisa Habari Halmashauri ya Wikaya ya Ukerewe Steven Msengi ulishushwa ukifuatiwa na jeneza lenye mwili wa Husna Mlanzi aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Luninga cha ITV.

Jeneza la nne kushushwa ni lenye mwili wa Anthony Chuwa aliyekuwa mwandishi wa kujitegemea akiandikia vyombo mbalimbali vya habari nchini uliofuatiwa na jrneza lenye mwili wa Jihari Shani wa Uhuru Digital ambaye pia aalikuwa askari polisi.

Jeneza lenye mwili wa Johari ulibebwa na askari polisi wa kike ikiwa ni sehemu ya taratibu za kijeshi.

Mwili wa mwisho kushushwa ulikuwa wa Paulo Silanga aliyekuwa dereva ofisi ya mkuu wa mkoa aliyekuwa anaendesha gari lililobeba wanahabari siku ya ajali.