Waziri Nape awasili Nyamagana kuongoza kuaga waliokufa ajali Simiyu

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akisaini kitabu cha maombolezo muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza inapofanyika shughuli ya kuaga miili ya waandishi watano waliofariki jana wakiwa kwenye ziara ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewasili katika uwanja wa michezo wa nyamagana kuongeza waombolezaji kuaga miili ya wanahabari watano na dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia katika ajali ya gari jana Januari 11.

Mwanza. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewasili katika uwanja wa michezo wa nyamagana kuongeza waombolezaji kuaga miili ya wanahabari watano na dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia katika ajali ya gari jana Januari 11.

Tayari miili ya marehemu imeshawasili uwanjani hapa kwa ajili ya kuaagwa kisha baadhi kusafirishwa kwenda Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro na mwingine ambao ni wa Husna Mlanzi wa ITV kuzikwa leo katika makaburi ya Kirumba jijini Mwanza.

Waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Shimanywile Wilaya ya Busega mkoani Mwanza baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso ni Johari Shani (Uhuru Digital), Husna Mlanzi (ITV), Anthony Chuwa (Habari Leo Digital), Abel Ngapemba (Ofisa Habari Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza) na Steven Msengi aliyekuwa Ofisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.

Dereva wa gari la Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza walilopanda wanahabari hao, Paulo Silanga naye alifariki dunia na anatarajiwa kuagwa leo.

Watu wengine wanane waliokuwa kwenye gari ndogo ya abiria aina ya Toyota Hiace pia walifariki papo hapo na hivyo kufanya jumla ya waliofariki kufikia watu 14.

Watakaosafirishwa kwenda Dar es Salaam ni Maofisa Habari wa Serikali Ngapemba na Msengi wakati Johari Shani wa Uhuru Digital atasafirishwa kwenda mkoani Arusha huku mwili wa Anthony Chuwa wa habari leo Digital utasafirishwa kwenda mkoa wa Kilimanjaro.