Wanahabari waliofia ajalini kuagwa uwanja wa Nyamagana

Muktasari:

Wanahabari watano na dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia katika ajali ya gari jana Januari 11 wanaagwa leo katika tukio linalofanyika uwanja wa michezo wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mwanza. Wanahabari watano na dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia katika ajali ya gari jana Januari 11 wanaagwa leo katika tukio linalofanyika uwanja wa michezo wa Nyamagana jijini Mwanza.

Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza inayoratibu shughuli zote za msiba huo ulioacha simanzi miongoni mwa waandishi na wadau wa habari ndani na nje ya nchi inaonyesha kuwa kufikia saa 3:00 asubuhi, miili ya marehemu itawasili uwanjani hapo kwa ajili ya dua na sala kutoka kwa viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali.

Waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Shimanywile Wilaya ya Busega mkoani Mwanza baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso ni Johari Shani (Uhuru Digital), Husna Mlanzi (ITV), Anthony Chuwa (Habari Leo Digital), Abel Ngapemba (Ofisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza) na Steven Msengi aliyekuwa Ofisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.

Dereva wa gari la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza walilopanda wanahabari hao, Paulo Silanga naye alifariki dunia na anatarajiwa kuagwa leo.

Watu wengine wanane waliokuwa kwenye gari ndogo ya abiria aina ya Toyota Hiace pia walifariki papo hapo na hivyo kufanya jumla ya waliofariki kufikia watu 14.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, dua na sala zitafuatiwa na salaam za rambirambi kutoka wazara yenye dhamana na masuala ya habari, wadau wa habari, ofisi ya mkuu wa mkoa na wawakilishi wa familia za marehemu.

Saa 5:00 asubuhi miili ya marehemu itakabidhiwa kwa familia ili kuruhusu shughuli rasmi ya kutoa heshima za mwisho zinazotarajiwa kukamilika saa 6:00 mchana.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko amesema baada ya heshima za mwisho, miili ya marehemu wanne inatarajiwa kusafirishwa kwa mazishi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam huku mmoja akitarajiwa kuzikwa leo jijini Mwanza.

Watakaosafishwa kwenda Dar es Salaam ni Maofisa Habari wa Serikali Ngapemba na Msengi wakati Johari Shani wa Uhuru Digital atasafirishwa kwenda mkoani Arusha huku mwili wa Anthony Chuwa wa habari leo Digital utasafirishwa kwenda mkoa wa Kilimanjaro.