Miili ya watu saba waliofariki ajali ya Chamwino kuzikwa leo

Muktasari:
Miili ya watu saba waliofariki katika ajali iliyohusisha gari na mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe jana inatarajiwa kuzikwa leo katika Kijiji cha Lugala, kata ya manzase wilayani Chamwino.
Dodoma. Miili ya watu saba waliofariki katika ajali iliyohusisha gari na mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe jana inatarajiwa kuzikwa leo katika Kijiji cha Lugala, kata ya manzase wilayani Chamwino.
Miili hiyo itaagwa kwenye ibada ya mazishi kuanzia saa 8 mchana katika Kanisa la Mtakatifu Marco wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 4, 2022 na Mwenyekiti wa Kijiji cha Manzase, Charles Kangwe amesema mazishi hayo yatafanyika katika makaburi ya kila familia kuanzia saa 10 alasiri.
“Kila familia itazika katika makaburi ya familia lakini kuagwa wataagwa kwa pamoja katika Kanisa la Mtakatifu Marco hapa hapa Manzase” amesema
Katika miili hiyo ipo familia ya mama (Helena Mkwawa) na watoto wake Irene Samson na Vaileth Samson, bibi (Eveline Masaka) na mjukuu wake Rehema Yohana na mmoja wa familia nyingine Isack Cherehani.