Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikopo umiza balaa, Gavana atoa tahadhari

Dar es Salaam. Wakati taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogomidogo zikiendelea kushamiri mitaani, tahadhari imetolewa kwa Serikali kuzimulika taasisi hizo kwa kile kinachodaiwa kutumia udhaifu wa jamii kutokuwa na elimu ya fedha kuwapa mikopo ya kinyonyaji.
Hata hivyo, taasisi hizo zinatajwa na wananchi kuwa kimbilio kutokana na urahisi wa utoaji mikopo, lakini zina riba kubwa zinazowaumiza.
Hayo yalielezwa wakati wa mjadala wa Twitter Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) uliokuwa na mada ‘ongezeko la taasisi za mikopo mitaani ni fursa au changamoto kwa jami’.
Akizungumza kwenye mjadala huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus alisema Watanzania wengi wameathirika na mikopo hiyo kwa sababu Serikali imeruhusu uwepo wake.
“Kama unakopa kwa ajili ya kufanya biashara ni nzuri zaidi kuliko kwa starehe, wakati mwingine wazazi wanalazimika kukopa kwa ajili ya kulipa ada, bahati mbaya shule zetu haziwavumilii wazazi kulipa ada, wanataka walipe Sh1 milioni kwa wakati mmoja,” alisema.
Mchambuzi wa uchumi, Oscar Mkude alisema lengo la kuanzishwa kwa taasisi hizo ndogo za fedha ni kusaidia wananchi, lakini kinachoonekana kufanyika sasa ni kuwanyonya wananchi kwa mikopo yenye riba kubwa na masharti magumu.
"Mikopo hii ilianzishwa kusaidia wakopaji wadogo, benki zinasaidia wakopaji wakubwa. Changamoto iliyopo ni kwamba inashindwa kufanikiwa kwa sababu wengi wanakopa kwa ajili ya kula.
“Bahati mbaya taasisi hizi haziulizi namna itakavyorejeshwa na ukiwa na cherehani au kitu chochote unakopeshwa, hivyo hiyo ni tofauti na benki,” alisema na kuongeza:
“Mikopo hii inajenga picha ya unyonyaji, kwani wameangalia faida na hawazingatii tena miongozo ya zamani ya kuuliza unafanyabiashara gani au kukupa elimu," alisema Mkude.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa masuala ya uchumi na mtaalamu wa benki, Cleopa Lema alisema watumishi wengi wa umma wanatakiwa kupewa elimu ya kisaikolojia, kwani asilimia kubwa wapo kwenye mikopo hiyo. “Katika watumishi wa umma 100 watumishi 20 wanaacha kadi zao kwenye hizo taasisi baada ya kukopa, hii ni kwa sababu wameshakopa benki na sasa hawakopesheki,” alisema.
Alisema mtu anaambiwa unakopeshwa Sh1 milioni riba asilimia tano, haulizi riba hiyo ni kwa muda gani, akianza kukatwa analalamika.
Lema alisema asilimia kubwa ya Watanzania uelewa kwenye mikopo ya biashara ni kwenye vitu vichache, lakini kwa watumishi kwa sababu anajua atakatwa kwenye mshahara hajui hatari atakayopitia.
 

Nani anakopa nini?

Akichangia mada hiyo, mhariri wa takwimu wa gazeti la Mwananchi, Halili Letea alisema Watanzania wengi wanaochukua mikopo hutumia fedha katika shughuli zisizo za uzalishaji, hivyo kuwawia vigumu katika urejeshaji.
Alisema ripoti ya utafiti wa ufuatiliaji wa kaya uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), iliyoonyesha matokeo ya namna Watanzania wanatumiaje fedha baada ya kukopa, asilimia 26.4 pekee ndio wanakopa kwa ajili ya kufanyia biashara.
“Asilimia 31.8 wanakopa kufanya matumizi ya kawaida kwa maana ya kununua chakula, asilimia 13 wanakopa kwa ajili ya elimu, yaani kulipa ada, asilimia 12.4 sawa na mtu mmoja kati ya 8 wanakopa kwa ajili ya matibabu, asilimia 11.7 kwa ajili ya kulipa kodi na kujikidhi kwenye makazi na asilimia 8.5 ni wakulima wanakopa kwa ajili ya kununua mbegu,” alisema Letea.
Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha wa Chama cha ACT Wazalendo, Ester Thomas alisema ni muhimu wananchi kuwezeshwa kupata mikopo ya halmashauri ambayo haitakuwa na riba.
Alisema mikopo hiyo maarufu kama ya asilimia 10 ipelekwe kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na itakwenda kumwezesha Mtanzania kuanzisha biashara na kuepukana na mikopo ya kausha damu.


Alichokisema Gavana

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na taasisi ndogo za ukopaji.
Alisema taasisi hizo zimegawanyika katika makundi matatu--- zile za ngazi ya jamii (vicoba), ngazi ya vyama vya ushirika (Saccos) na kampuni au mtu binafsi ambazo haziruhusiwi kukusanya dhamana.
Tutuba alisema kuna vigezo wameviweka ambavyo kwanza ni asajiliwe na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), huku akieleza inapaswa kuwa taasisi inayotambulika na kufahamika.
“Lazima awe na ofisi na chumba wanachotolea mikopo, ili mtu akiwa na malalamiko anatakiwa kuyaleta na wayafanyie kazi na benki wanapopita kukagua wayakute na waanze kufuatilia,” alisema.
Gavana huyo alisema kigezo kingine ni lazima wawe na mtaji kuanzia Sh20 milioni hadi Sh20 bilioni na zaidi ya hapo, anapotoa huduma anatakiwa awe na andiko la kisera linaloelezea huduma anazotoa.
Alisema kwa wale wenye kampuni, wakisoma kwenye sheria ya makampuni, kuna kitu kinaitwa mkataba na vifungu vya ushirika.
“Kupitia mkataba huo anatakiwa aeleza anatoa mikopo na anaendesha shughuli gani za halali zinamfanya asajiliwe kama kampuni,” alisema.
Tutuba alieleza hata wakati wanapowasilisha maombi, ni lazima aonyeshe huduma atakazozitoa na sera yake. Pia atoe taarifa, kufunga hesabu na kulipa kodi.
Alisema baada ya kujisajili ndipo taasisi hiyo inatoa leseni ambayo kunakuwa na masharti.
“Unatakiwa kutoa mikopo riba isizidi asilimia 3.5 kwa mwezi. Kuna baadhi wanavuka kiwango hicho na wengine unakuta hata hawajasajiliwa,” alisema.
Alisema bahati mbaya watu na baadhi ya wafanyabiashara wakitangaziwa sehemu kuna mikopo wanajipeleka bila kuulizia na kujua masharti yake.
“Tunatoa leseni na tunawataka waweke hadharani masharti kusudi mtu anayeenda kukopa ajue riba ni kiasi gani na anavyokopa atakaporejesha ni kiasi gani,” alisema.
Tuzo Mapunda, Elizabeth Edward na Devotha Kihwelo