Milioni 400 za Uviko-19 zakwama kutumika Ngorongoro

Friday February 04 2022
uviko pic
By Janeth Mushi

Ngorongoro. Jumla ya Sh 400 milioni  za miradi inayojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa wastani wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19,zilizokuwa zitumike  kujenga vyumba 16 vya madarasa na bweni moja zimeshindwa kutumika baada ya kukosekana kibali cha ujenzi.

 Fedha hizo zilizotolewa na serikali zilipangwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo na bweni hilo katika Tarafa ya Ngorongoro,wilayani hapa mkoa wa Arusha.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo katika kijiji cha Nainokanoka,wananchi hao wameeleza kusikitishwa na kitendo cha serikali kutoa fedha hizo na kushindwa kutumika kwa ajili ya miradi hiyo ikiwemo wa elimu na afya.

Aidha wananchi hao wamemuomba Rais Samia Suluhu kuangalia upya mgogoro kati ya jamii hiyo ya kifugaji na wahifadhi katika eneo hilo ili waweze kujua hatma yao.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho Esupat Melejii ,amesema wanawake wamekuwa mstari wa mbele kuwafundisha watoto kutunza mazingira na kuwa hawawezi kuharibu uhifadhi.

"Mwanamke ndiye mwalimu wa kwanza kumfunza mtoto asiharibu mazingira,ndivyo tulivyowafunza na sisi tulifundishwa na bibi zetu ndiyo maana mnaona Ngorongoro inang'ara,tunatunza wanyamapori kwa ajili ya vizazi vyetu na vijavyo,"alisema

Advertisement

Naye mzee wa mila maarufu kama Laigwanan,Sembeta Ngoitiko,alisema kukosekana kwa fedha hizo za kuendeleza miradi ya maendeleo kutaathiri jamii hiyo kwa kiasi kikubwa.

"Hii imetuathiri sana ukiangalia kuna shule ndani ya tarafa ya Ngorongoro ambazo zimetengewa fedha nyingi kwa ajili ya kuongeza madarasa,zahanati kuna mengine kwa ajili ya kuendeleza mifugo,tutaathirika pakubwa magonjwa ya mifugo yatakuwa ni mengi ya binadamu na watoto wetu watarudi hawajui kusoma kwa kukosa madarasa,"

Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro,Edward Maura,alisema katika mpangilio wa uanzishwaji wa hifadhi hiyo ni pamoja na kuendeleza wenyeji na kudai kuwa baadhi ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza Ngorongoro wamekuwa wakipotosha.

Maura ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nainokanoka,alisema katika kijiji hicho Kituo cha afya Serikali imetenga Sh 580 milioni na kudai kuwa iko kwenye akaunti ya halmashauri kwa zaidi ya miezi saba baada ya kibali kukosekana.

“Mimi hapa ni diwani wa Kata nawahudumia wananchi zaidi ya 21,000 sasa hivi naenda kula posho tu kwa sababu  Serikali kupitia Wizara mbalimbali ikiwemo afya na maji,zinatenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Ngorongoro lakini wanatunyima haki kwa kuzuia kibali,watoto wetu wasiwe na madarasa.

“Tunataka serikali yetu kupitia CCM,ijue kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano inataka haki itendwe kwa watanzania wote,haiwezekani shule ijengwe Arumeru,Mtwara,Songea halafu unafika Ngorongoro unatunyima haki ya kupata elimu," amesema

Naye Elizabeth Makamelo mkazi wa Kijiji cha Nayobi,alisema kukosekana kwa vibali kunasababisha kukosa kwa huduma bora ikiwemo maboresho ya huduma za afya na sekta ya elimu.

Akizungumzia fedha hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Jumaa Mhina, amesema kuwa serikali imetoa zaidi ya Sh 1.85 bilioni na kati ya hizo Sh 400 milioni ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 16.

Amesema kila darasa lingejengwa kwa Sh 20 milioni huku bajeti hiyo ikitenga Sh 80 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Tarafa hiyo ya Ngorongoro.

"Kati ya madarasa hayo 12 yangekuwa ya sekondari na manne yalikuwa ya shule za msingi na bweni moja,ambayo yalitakiwa kumalizika kabla ya mwezi Januari mwaka huu,"alisema

Amesema fedha hizo hazijaweza kutumika hadi sasa kwani Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA),hawajatoa kibali kwa ajili ya ujenzi huo hadi sasa.

“Tarafa ya Ngorongoro ukitaka kufanya shughuli yoyote lazima upate kibali cha mamlaka na halmashauri haikupata kibali kwahiyo madarasa ya Uviko- 19 hayakujengwa moaka sasa,"amesema

Advertisement