Miti 2,100 yapandwa mashuleni kuadhimisha miaka 60 ya Muungano

Muktasari:

  •  Malengo ya kupanda miti ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa kutunza mazingira.

Dar es Salaam. Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imepanda miti 2,100  katika shule mbalimbali za jijini hapa, ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano yatakayofika kilele chake Aprili 26, 2024.

Sambamba na hilo pia ni katika mwendelezo wa kampeni ya wizara hiyo ya  'Soma na Mti' iliyoanzishwa na Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, Suleiman Jafo, lengo likiwa kupanda miti milioni 14.5 kwa mwaka katika hule zote nchini.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Aprili 19, 2024 na Balozi wa Mazingira kutoka Wizara hiyo, Veronica Massawe, alipomwakilisha Waziri Jafo kupanda miti na wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Kigezi iliyopo Kata ya Chanika, Wilaya ya Ilala.

Veronica amesema shule hiyo imepatiwa miti  300 ikitanguliwa na Shule ya Sekondari wasichana Dar es Salaam iliyopo Wilaya ya Ubungo (miti 500), Shule ya Msingi Dar es Salaam miti 800 na Shule ya Ally Hapi iliyopo Wilaya ya Kinondoni ambako miti 500 imepandwa.

"Malengo ya kupanda miti hii ukiacha kutumia kama fursa kuwaeleza wanafunzi umuhimu wa Muungano, lakini pia kuwajengea tabia ya kutunza mazingira kwa kupanda miti," amesema

Akieleza mwitikio wa jamii katika kampeni hiyo amesema mzuri na kueleza faida haitakuwa tu kwa wanafunzi na walimu, bali na jamii kwa ujumla ukizingatia miti inayopandwa ni ya matunda.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kigezi, Ladislaus Mutanda, amesema wanajivunia shule yao kuchaguliwa katika kampeni hiyo.

"Ahadi yangu kwa Waziri ni kuitunza miti mpaka ikiue kama ilivyotarajiwa kwa kuwa kupata miti hii ni faraja kwetu, ukizingatia huko nyuma kuna iliyoanguka baada ya kunyesha mvua nyingi," amesema Mwalimu Mutanda.

Kwa upande wao wanafunzi akiwemo Caren Mrema amesema amejifunza kitu kipya katika upandaji miti ikiwemo namna ya kuushika kabla ya kuupanda na njia sahihi.

Joshua Mwakyoma, amesema miti ni muhimu kupandwa ili kukabiliana na uharibu wa mazingira lakini pia kusaidia katika kuleta mvua.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kigezi, Seleman Kiumbo amesema kampeni hiyo ni nzuri ukizingatia kwa sasa dunia inapambana na mabadiliko ya tabianchi.