Miundombinu bora yaipaisha Mlele matokeo darasa la saba

Angalia hapa matokeo ya Darasa la Saba

Muktasari:

Halmashauri ya wilaya ya Mlele  ndani ya miaka mitano imejikuta ikiingia kwenye nafasi ya kumi bora kitaifa mara mbili na imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kimkoa.

Katavi. Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Alexis Kagunze amesema kilichowafanya washike  nafasi  ya kumi kati ya Halmashauri bora kitaifa katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu, kumetokana na uongozi  kuboresha miundombinu ya shule.

Pia amesema mbinu za ufundishaji na kutoa motisha kwa walimu ni moja ya sababu kubwa zilizosaidia.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana Jumamosi jioni Novemba 21, 2020 Kagunze alitaja mbinu nyingine waliyoitumia  wakati wa likizo ya miezi mitatu ya  Covid - 19 ni kwa uongozi kwa kushirikiana na walimu kutengeneza maswali  kila wiki na kuwagawia wanafunzi kupitia ofisi za Maofisa  Watendaji  na Waratibu elimu kata kupitia kwa wazazi waliokuwa wakiwapatia watoto wao nyumbani.

“Wanafunzi wanajibu na kurejesha katika ofisi hizo,  walimu walichukua kusahihisha na  kutoa majibu kwa utaratibu huo, corona ilipoondoka  wanafunzi walirejea shuleni wakapatiwa majibu yao mazuri, wakaendelea kufanya mazoezi,” alisema Kagunze.

Kuhusu kuwapa motisha na  haki zao stahiki  walimu, alisema wamekuwa wakitoa  malipo ya likizo na uhamisho kwa muda muafaka ikiwamo kuwapatia viburudisho mbalimbali,  hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa  walimu kuwa na morali ya kufundisha.

“Lakini wanafunzi  walijiandaa vizuri, baada ya kupewa mafunzo ya Necta kwamba kuna mabadiliko ya namna ya kufanya mitihani itakavyotungwa, tuliwajulisha walimu wakuu na  taaluma ili wabadilike waendane na wakati, tumeboresha miundombinu ya shule mfano tumetengeneza  madawati ya kutosha, madarasa mazuri, vyoo vya kisasa  hadi vya ziada vipo,” alisema Kagunze.