Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mjasiriamali alivyogeukia biashara ya mkaa mbadala

Mbunifu wa mkaa mbadala na majiko banifu eneo la Masanga Manispaa ya Kigoma Ujiji, Godlove Kamuntu (kulia) akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye majiko aliyotengeneza kwa ajili ya kupikia kwa matumizi ya mkaa huo. Picha na Happiness Tesha

Kigoma. "Nilikuwa nimebeba mkaa kwenye gari yangu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kisha nikasimamishwa na watu wa Maliasili wakiwa wanataka kuona kibali cha mkaa huo," anasimulia Godlove Kamuntu, mkazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

"Kwa bahati mbaya sikuwa na kibali, ndipo waliponiambia kuwa Serikali imepiga marufuku ukataji miti kwa ajili ya kuzalisha mkaa. Wakaninyang’anya. Tangu siku ile wakawa wamenipa somo kubwa sana."

Mjasiriamali huyo mwenye kiwanda kidogo cha kuzalisha mkaa mbadala, vumbi la maranda ya mbao na mabaki ya nyasi kavu, vinavyotumika kama malighafi ya kutengeneza mkaa huo.

“Nilibuni mashine ya kutengeneza mkaa huo kwanza kabla ya kuwaza kubuni mkaa wenyewe utakuaje na nilifanikiwa kuanza kutengeneza mtambo wa kutengeneza mkaa wa tani moja kwa siku, hadi sasa nimefikia kutengeneza zaidi ya tani saba kwa siku,”alisema Kamuntu ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Byoma Engineering inayotengeneza mitambo mbalimbali, iliyopo Masanga, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Alisema alifikiria kitu gani kinaweza kutengeneza mkaa mbadala na aligundua chenga za mkaa zingekuwa suluhu.

Suala la malighafi hiyo kuwa ngumu, anasema kulimfanya ahamie kwenye maranda ya mbao, nyasi pamoja na pumba za mpunga.

Kamuntu alisema kuzalisha mkaa huo kunapitia hatua mbalimbali ndani ya siku saba mpaka kukamilika kwake.

“Baada ya kubuni mkaa wetu tulifanya majaribio kwenye majiko ya mkaa wa kawaida mkaa ulifanya vizuri lakini tulivyobuni majiko yetu mkaa huo ulifanya vizuri zaidi ya mkaa wa miti,”alisema Kamuntu.


Umuhimu wa mkaa mbadala

Akizungumzia makaa huo, alisema unaweza kuwaka kwa saa tano hadi sita bila kuongeza na hivyo kuwezesha kulipa kwa muda mrefu.

Kilo moja ya mkaa huo inauzwa Sh400 na inaweza kupika kutwa nzima na aina tofauti hadi tatu za chakula kama maharagwe bila kuongeza mkaa kwa familia ya watu wachache (chini wa watano) ikilinganishwa na fungu la mkaa wa kawaida wa Sh1,000 ambao hauwezi kufanya hivyo.

 "Kama nilivyokuwa mimi bado uelewa ni mdogo sana baina ya watu, hivyo tunaendelea kuhamasishana juu ya madhara ya ukataji miti kwa ajili ya nishati ya kupikia ili kupunguza athari katika mazingira,”alisema Kamuntu.

Alisema sababu kubwa ya watu kutotumia nishati mbadala ni urahisi wa upatikanaji wa nishati hiyo.

"Mkoa bado una maeneo makubwa ya misitu na miti ya kutosha hivyo watu wengi wana uwezo kuifikia misitu hiyo na kupata kuni na mkaa,” alisema Kamuntu.

Alisema ili elimu hiyo ifike mbali zaidi, wanahitaji vijana wengi wa kuwafundisha kazi hiyo ili nao waende wakatoe ujuzi huo kwa wengine na hatimaye kila mmoja atumie mkaa mbadala kulinda mazingira.

Kamuntu alisema anakaribisha wadau mbalimbali ili waunganishe nguvu katika kuhakikisha elimu na mkaa huo mbadala unawafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma, kwa kuwa malengo yake ni kujitangaza kimataifa na bidhaa yake kufika mbali zaidi.


Watumiaji wa mkaa

Mkazi wa Kata ya Mwanga, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Success Halisi alisema ameanza kutumia mkaa huo miezi sita sasa na ameona kuna utofauti na wa miti kwa gharama na kiafya.

“Mkaa wa miti nilikuwa nikinunua wa buku (Sh1,000) nikitenga maharagwe siwezi kuivisha, ilikuwa inanilazimu ninunue mkaa wa Sh2,000 kuivisha na kupika wali lakini mkaa huu mbadala naweza kununua kilo moja kwa Sh400 na nikafanya yote hayo na kubaki,hivyo umetupungungia gharama za maisha,”alisema Halisi.

Neema Lameck, mkazi wa Masanga Manispaa ya Kigoma Ujiji, alisema ni miezi miwili sasa tangu aanze kutumia mkaa mbadala na umemrahisishia kuokoa muda.

“Hausumbui kuwasha na ukiwaka unawaka kama gesi, hivyo napika haraka zaidi hata kama nitachelewa kurudi nyumbani kutoka kwenye shughuli zangu,”alisema Neema.

Alisema, awali alikuwa akinunua mkaa gunia kwa Sh30,000 hadi 40,000 na alikuwa anatumia kwa miezi miwili, lakini tangu aanze kutumia mkaa mbadala ananunua mkaa wa Sh7,000 na anakaa nao zaidi ya wiki moja.

Neema aliwashauri kina mama wapende kujaribu vitu na wasikariri kuwa mkaa ni mmoja tu, kwa kuwa, mkaa mbadala nao unafanya kazi zaidi ya wa kawaida na unatunza mazingira hasa ukitumia na jiko lake .


Serikali yataja changamoto, mikakati

Kaimu Ofisa Misitu na Mazingira Mkoa wa Kigoma, George Gwalema alisema mkakati ni kutoa elimu kwa jamii kuanzia ngazi za juu hadi chini ili kuhakikisha wanaona umuhimu wa kutumia nishati mbadala.

Gwalema alisema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha matumizi ya nishati mbadala ikiwamo mkaa huku shule 17 zikiwezeshwa kutumia majiko ya mkaa mbadala kupitia Mradi wa Pamoja wa Kigoma (KJP).

“Pia, tumewajengea uwezo maofisa zaidi ya 28 wa halmashauri, taasisi mbalimbali 15 zilizopo na vikundi 52 vya wafanyabiashara wadogo kwenye eneo la mkaa mbadala,” alisema Gwalema.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye anakiri kuwepo kwa uharibifu wa mazingira kwa kukata miti kwa ajili ya mbao, kuni na mkaa.

Andengenye alisema kwa sasa kuna ubunifu wa mkaa mbadala uliokuja kutatua changamoto za kiuchumi pamoja na kiafya kwa kuwa hakuna madhara kwa mtumiaji kutokana na kutokuwa na moshi, hivyo kila mtu aweze kuona umuhimu wa kutumia mkaa huo.

“Mkaa wa miti umetuumiza kwa muda mrefu kiuchumi kwani gharama zake ziko juu ukilinganisha na huu unaotengenezwa hapa ambao hautumii miti, mkaa wa miti umeumiza pia mazingira pamoja na watumiaji ambao wengi ni kina mama na kuhatarisha afya zao,”alisema Andengenye alipotembelea Kiwanda cha Kamuntu.

Alisema Serikali inaangalia namna ya kushirikiana na wabunifu kupitia taasisi zake kwa kuwa kila taasisi yenye watu zaidi ya 100 inatakiwa iachane na kuni na mkaa.


Wakala wa Huduma za Misitu

Mhifadhi Mwandamizi wa Misitu wilaya ya Kigoma kutoka Wakala wa Huduma za MisituTanzania (TFS), Asheri Petro alisema miti inakatwa sana kwa sababu ya kupanua mashamba na mkaa.

Petro alisema uzalishaji wa mkaa wa kukata miti ni gharama ukilinganisha na mkaa mbadala kwa kuwa, mzalishaji anatakiwa kulipia Sh250 kwa Serikali, kulipa ushuru wa asilimia tano kwa halmashauri husika, gharama nyingine za uzalishaji na gharama za usafirishaji.

“Mkaa wa miti una gharama kidogo katika uzalishaji ukilinganisha na huu mkaa mbadala hauna gharama kwa sababu vitu vya kutengenezea mkaa huo vinapatikana kwenye mazingira yetu ya kila siku hivyo kufanya kuwa rahisi kutengeneza,”alisema Petro.


Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917