Prime
Mjengo mpya wa Chadema
Nyumba inayotarajiwa kuwa ofisi za Chadema iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Na mpiga picha wetu
Dar es Salaam. Miaka 30 tangu kupata usajili wa kudumu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kuhamia kwenye jengo lake jipya litakalokuwa makao yake makuu.
Jengo hilo la ghorofa moja lililopo Mikocheni, Dar es Salaam, lina vyumba zaidi 10.
Inaelezwa kuwa jengo hilo limenunuliwa na kukarabatiwa kwa zaidi ya Sh1.5 bilioni kati ya Sh2 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya majengo ya chama hicho Tanzania Bara na Zanzibar.
Taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza ofisi hizo zitaanza kutumika mwezi ujao na kuyafanya makao makuu ya Chadema yaliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni kubakia kwenye vitabu vya historia.
Chadema ilihamia ofisi za Mtaa wa Ufipa mwaka 2000 na katika siku za hivi karibuni viongozi wake walikuwa wakisakamwa kwa kushindwa kujenga ofisi yenye hadhi inayoendana na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Licha ya kusakamwa huko, viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, John Mnyika walikuwa wakisema jengo si kipaumbele chao, bali kukiimarisha chama hicho mikoani na kwenye mioyo ya watu.
Kejeli na kusakamwa kuliongezeka mwaka jana baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kilichoanzishwa mwaka 2014 kuzindua jengo lake jipya ambalo ni makao makuu ya chama, Magomeni, jijini Dar es Salaaam.
Mwonekano wa jengo
Jengo jipya la Chadema lina mwenekano wa kisasa na mandhari nzuri zaidi kulinganisha na majengo ya vyama vingine vya upinzani.
Limeezekwa kwa vigae, lina bustani na vitofali vya simenti (pavings). Pia lina eneo la maegesho ya magari ya viongozi, wageni pamoja na kumbi za mikutano.
Inaelezwa vyumba hivyo vitatumika kwa ofisi za viongozi wakuu wa Chadema na mabaraza ya chama hicho.
Mmoja wa viongozi wa Chadema aliieleza Mwananchi, kuwa hivi sasa yanafanyika marekebisho madogo, ikiwamo kupakwa rangi za chama hicho kwa nje.
Mwenyekiti wa kamati ndogo iliyoundwa kusimamia na kuratibu mchakato wa ununuzi wa majengo ya ofisi za Chadema Tanzania Bara na Unguja, Ezekiah Wenje alisema kila kitu kimekamilika, kilichobaki ni kuhamia katika ofisi hizo.
“Tunachosubiri ni kuwaita waandishi wa habari, ili tuwaonyeshe ofisi yetu mpya, kila kitu kimeshakamilika. Ofisi ipo katika jina letu hadi sasa baada ya kukamilisha taratibu zote. Subiri siku hiyo tutawaita si ninyi tu, hadi Msajili wa vyama vya siasa,” alisema Wenje alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia suala hilo.
Alisema pia watawaalika viongozi wa vyama vingine vya siasa na kwamba, itakuwa hafla ya kukakata na shoka.
“Wanahabari tutawatembeza mtaona mazingira yote ya ofisi yetu mpya. Chadema inafikiria mambo makubwa yanayohitaji utulivu, sasa mazingira ya ofisi yapo maeneo yenye utulivu,” alisema.
Hata hivyo, Wenje ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, hakutaka kuweka wazi mazingira ya ofisi ilivyo au jengo la ghorofa ngapi, mtaa inapopatikana na gharama zake, badala yake alimtaka mwandishi kusubiri siku ya uzinduzi rasmi.
“Ofisi tutaizindua Julai (mwezi huu), inawezekana ikawa tarehe za katikati, subirini very soon (siku za karibuni) mtaona jengo letu la kisasa. Sitaki nimalize utamu wa jambo hili, narudia tena subirini tu msiwe na haraka, tunataka iwe ‘surprise’ kwa Watanzania,” alisema.
Wenje, aliyewahi kuwa mbunge wa Nyamagana mkoani Mwanza kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, alisema mchakato wa ofisi ndogo ya makao kuu ya Chadema, Zanzibar unaendelea na upo mbioni kukamilika.
Ofisi za Ufipa
Katika hatua nyingine, Wenje alisema majengo ya ofisi za chama hicho zilizopo Ufipa zenye majengo mawili zitabakia kuwa makumbusho na kumbukumbu muhimu kwao.
“Ufipa itabaki kama sehemu yetu ya makumbusho, ndipo tulipoanzia maisha yetu, patakuwa ndiyo sehemu ya historia ya Chadema. Ofisi hazitauzwa wala… bali itakuwa ni maktaba itakayobeba kumbukumbu nyingi, safari ya milima na mabonde ya Chadema hadi kilipo sasa,” alisema Wenje ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Mkurugenzi wa mawasiliano, itikadi, uenezi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia mkakati wa kuhamia ofisi mpya, hakuwa tayari kuelezea suala hilo, akisisitiza wakati ukifika umma utajulishwa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa uamuzi wa ununuzi wa majengo ya ofisi mbili za makao makuu ya Chadema Tanzania Bara na Zanzibar ulibarikiwa baada ya Wenje kuwasilisha mapendekezo mbele ya kikao cha Kamati Kuu kilichoketi jijini Dar es Salaam Aprili 10, mwaka huu.
Wakati huo, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina alisema,“…zilikuja nyumba kama nne hivi, zilikuwa za Masaki na Mikocheni, lakini tumechukua ya Mikocheni.
“Yatakuwa makao makuu ya kisasa sana, tunataka kuondokana na zile propaganda kuhusu ofisi. Sh2 bilioni zimetengwa kwa ofisi za Tanzania Bara na kati ya Sh300-400 milioni kwa ofisi za Zanzibar, kila kitu kinakwenda vizuri. Ila makao makuu ni yenye hadhi hasa.”