Mjumbe wa Baraza la Ardhi aibua vilio kesi ya wapangaji 52 Kariakoo

Baadhi ya wafanyabiashara walilopanga vyumba katika jengo la biashara, Kariakoo, jijini Dar es Salaam wakiwa katika Baraza la Ardhi  Mmazi Mmoja jijini humo baada ya kufanya majadiliano na mmiliki wa jengo hilo jana Machi 7, 2024. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Sakata la wapangaji 52 wa Kariakoo lachukua sura mpya, baada ya mmoja wa wajumbe wa Baraza la Ardhi kuangua kililo mbele ya Baraza akidai amepata hisia kali kutokana na malalamiko ya wapangaji hao.

Dar es Salaam. Mmoja wa wajumbe wa Baraza la Ardhi la Kata ya Kariakoo, Hamisi Bushiri Pazi ameangua vilio mbele ya wajumbe wenzake, wakati wa usikilizaji wa shauri la wafanyabiashara 52 wanaopinga kuhamishwa katika jengo walilopanga.

Wafanyabiashara hao wamemshtaki mmiliki mpya wa jengo hilo la ghorofa moja lililopo block namba 18, Plot 4 l mtaa wa Mchikichi, Kariakoo, kampuni ya Phinison Investment Limited, wakipinga uamuzi wake wa kutaka kuwaondoa kabla ya mikataba yao kuisha.

Jengo hilo lenye flemu zaidi ya 42 za maduka, awali lilikuwa linamilikiwa na Kaisi Hamis Ally lakini baada ya kampuni ya Phinison kulinunua, mmiliki mpya aliwapa wapangaji notisi ya siku tatu jambo ambalo hawakukubaliana nalo ndipo wakafungua shauri hilo.

Leo, Machi 12, 2024 shauri hilo liliitwa kwa ajili ya  usikilizwaji baina ya wapangaji, mmiliki wa zamani wa jengo hilo Kais Ally na mmiliki mpya, George Phinison.

Katika usikilizwaji huo, Kaisi alipaswa kulieleza baraza hilo kama anawatambua wapangaji hao na hatima ya vyumba vyao vya kupanga.

Wakati wa usikilizwaji huo, Pazi alipewa nafasi na baraza hilo kutoa maoni kuhusu mgogoro huo. Katika maoni yake, naye akapendekeza baraza litoe barua kwa wapangaji hao waende katika hatua ya mbele.

 “Mimi naona baraza liwape barua hawa wafanyabiashara waende mahakamani ili kuondoa manunguniko kwa sababu wanaweza kuja kusema Baraza la Ardhi la Kata ya Kariakoo linawapendelea watu wenye hela,” alisema Pazi na kuanza kulia huku akijifunika uso kwa kutumia mikono yake.

Ushauri huo wa Pazi umeungwa mkono na wapangaji hao kwa kumpigia makofi, lakini wakati wakiendelea kufurahia mapendekezo hayo, Pazi alianza kulia kwa sauti.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wapangaji hao nao wakaanza kulia naye huku  mmoja wao, Efatha Shao akaenda kumkumbatia kumbembeleza anyamaze kulia, huku naye akiangua kilio kwa machozi na sauti.

Baadaye alipoulizwa na Mwananchi sababu za kuangua kilio hicho, Pazi amesema alishindwa kuvumilia kutokana na malalamiko ya wapangaji hao kuhusu hatima yao na biashara zao.

Kutokana na mvutano wa pande zote mbili na mapendekezo hayo aliyoyatoa pazi, mwenyekiti wa Baraza hilo, Daud Simba amekubaliana nayo na akaahirisha shauri hilo hadi Machi 14, 2024 ambapo wapangaji hao watapewa barua waende katika hatua ya juu.

“Kwa kuwa mmetaka jambo lenu liende mbele, basi mje Alhamisi ili mchukue barua mwende mbele,” amesema Simba


Hali ilivyokuwa

Awali kabla ya kilio hicho, Baraza hilo lilitoa nafasi kwa mmiliki wa awali na wa sasa kueleza namna walivyouziana jengo hilo.

Phinison (57) aliyeambatana na mke wake, Salome Mgaya maarufu kama mama Bonge, amedai kuwa alinunua nyumba hiyo kutoka kwa Kais Ally, Oktoba 10, 2023.

“Mkataba wangu nimeingia na Kais Ally na mkataba wenyewe huu hapa,” amesema Phinison, huku akimpatia mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo waupitie.

Mmoja wa wajumbe wa Baraza alimhoji maswali kadhaa mnunuzi huyo na ifuatayo ilikuwa ni sehemu ya mahojiano hayo.

Mjumbe: George baada ya kununua nyumba hiyo, ulimlipa Kais hela mkononi au ulimwingizia Benki?

George: Nilimpa cash (taslimu) mkononi na nyingine nilimwingizia benki. Sasa sifahamu kwa nini Kais alienda kuchukua pesa za wapangaji wake na kusanishiana mikataba nao Novemba 8, 2023, wakati mimi na yeye tuliuziana Oktoba 10, 2023.

Mjumbe: Sasa unampaje fedha hizo mkononi?

George: Nyingine nilimwingizia benki.

Baada ya majibu hayo, wapangaji walihoji kwa nini George ampatie pesa nyingi mkononi badala ya kumwekea benki? Wengine walienda mbali zaidi na kudai kuwa wanataka alete taarifa ya kibenki ili waone fedha hizo aliziingiza tarehe ngapi.

Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti wa baraza hilo aliingilia kati na kuwataka, wapangaji hao kutulia kwa kuwa yeye ndiye anaendesha shauri hilo na atatoa nafasi ya kuzungumza kwa wapangaji hao, hivyo wampe nafasi George kueleza jinsi alivyosaini mkataba wa mauziano ya nyumba hiyo.

Baada ya kumaliza kujieleza, Baraza hilo lilimpa Kaisi nafasi kuelezea mkataba na jinsi atakavyowasaidia kumalizia mkataba wao.

Kais amesema maneno aliyotoa George si sahihi, japo hakumbuki tarehe rasmi ya kuuziana nyumba hiyo lakini anachokumbuka ni kuwa aliuza jengo hilo likiwa tayari na wapangaji.

Kais naye alihojiwa na wajumbe wa Baraza hilo na sehemu ya mahojiano ilikuwa kama ifutavyo;

Mjumbe, Kaisi mauziano mlifanya lini?

Kaisi: Sikumbuki maana ninao mkataba upo kwa mwanasheria.

Mjumbe: Tunataka tuone mkataba na wewe kabla ya kutoa maamuzi

Kaisi: Sawa

Mjumbe: Novemba 8, 2023 ulienda kuchukua hela za wapangaji wakati nyumba umeshauza.

Kaisi: Mkataba anao mwanasheria wangu.

Mwenyekiti: Njoo na mkataba wako, Alhamisi ili tuweze kuiangalia na kutoa uamuzi

Kaisi: Sawa.

Mjumbe: Kais ni kweli ulimuuzia nyumba?

Kaisi: Ndiyo, nilimuuzia.

Wapangaji: Tunaomba apigiwe wakili wake kama yupo mkataba ufuatwe maana ofisi yake ipo Kariakoo ,ni karibu na hapa.

Kaisi: Wakili hayupo ofisi, yupo mahakamani.

Mwenyekiti: Basi uje nao Alhamisi ili tuuone na kujua uliuza lini nyumba hiyo.

Baada ya kutokea kwa hali hiyo, wapangaji walihoji sababu ya nyumba kuuzwa huku wakiwemo ndani.

Mmoja wa wapangaji hao, Hubert Maleko amesema George alitakiwa apewe nyumba ikiwa haina wapangaji, sasa kwa nini alikabidhiwa nyumba ikiwa na wapangaji

Maleko baada ya kuuliza swali hilo, ndipo mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Pazi alipotoa mapendekezo yake kuwa wapangaji hao wapewe barua na baraza ili waende mahakamani.