Wapangaji 52 Kariakoo wamburuza mwenye nyumba Baraza la Ardhi

Muktasari:

  • Wapangaji hao wanataka mmiliki huyo asubiri mpaka kodi yao iishe, ndipo waondoke afanye ukarabati wa jengo hilo kama anavyotaka kufanya.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara 52 wa Kariakoo jijini Da es Salaam wamemshtaki mmiliki wa jengo walilopanga kwa ajili ya biashara wakipinga uamuzi wake wa kutaka kuwandoa kabla ya mikataba yao kwisha.

Jengo hilo la ghorofa moja, lililopo Mtaa wa Mchikichi Kariakoo lenye flemu zaidi ya 42 za maduka, awali lilikuwa linamilikiwa na Kaisi Hamis Ally ambaye baadaye aliliuza kwa kampuni ya Phinison Investment Limited ambaye ndiye mmiliki kwa sasa.

Baada ya kulinunua jengo hilo, Mkurugenzi wa kampuni ya Phinison, Salome Mgaya maarufu kama Mama Bonge, Februari 25, 2024 aliwapa taarifa ya mdomo wapangaji wake akiwataka wahame ndani ya siku tatu akidai anataka kulifanyia ukarabati.

Mama bonge aliwataka wapangaji hao kuhama katika jengo hilo Februari 28, 2024 lakini wapangaji hao hawakukubaliana na uamuzi huo, ndipo wakafungua malalamiko yao katika Baraza hilo la Ardhi la kata dhidi ya kampuni hiyo na mmiliki wa awali kupinga uamuzi huo.

Katika shauri hilo namba 13 la mwaka 2024 lililofunguliwa na Hubert Edwin Maleko kwa niaba ya wenzake 51, wapangaji hao wanadai kuwa uamuzi wa mmiliki wa jengo hilo kuwataka waondoke ndani ya muda huo ni kinyume cha mikataba yao.

Wapangaji hao, wanadai kuwa mmiliki huyo mpya wa jengo hilo anakiuka utaratibu kwa kuwa wao wana mikataba halali na bado haijaisha muda wake.

Shauri hilo lililonguliwa Februri 27, 2024, lilisikilizwa tena jana Alhamisi Machi 7, 2024 na mmiliki huyo akawapa miezi miwili badala ya siku tatu za awali.

Pia, amesema baada ya ukarabati watarudi lakini kwa kodi mpya, yaani kodi itaongezeka, kutoka waliyokuwa wanalipa ya Sh840, 000 hadi Sh1.5 milioni kwa mwezi, hivyo watalazimika kuongezea kwenye kodi iliyosalia.

Hata hivyo, wapangaji hao wamekataa muda huo wa miezi miwili wakitaka asubiri mikataba yao iishe na kwamba hawahitaji kulipwa fidia.

Kutokana na mvutano huo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Daudi Simba ameliahirisha shauri hilo hadi Machi 12, 2024 kwa ajili ya kuendelea na majadiliano na ametoa hati ya kumuita katika baraza hilo, mmiliki wa zamani wa jengo hilo ambaye ni Kaisi Ally.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutoka kwenye majadiliano hayo, Maleko amesema mkataba huo walioingia na mmiliki wa zamani, Kaisi Hamis Ally, walilipa kodi yao ya mwaka mmoja kuanzia Novemba 9, 2023 hadi Novemba 8, 2024.

Pia, miongoni wapangaji hao wapo waliolipa kodi ya miezi sita ambayo inatarajia kuisha Julai mwaka huu.

Amesema kuwa katika flemu hizo za maduka, mpangaji mmoja analipa kodi ya Sh840,000 kwa mwezi mmoja, huku mpangaji wa stoo analipa Sh250,000 kwa mwezi, wakati mpangaji wa vigoro (kizimba) analipa Sh 300,000 kwa mwezi na kodi hizo wanatakiwa kulipa kwa miezi sita au mwaka mmoja.

“Mimi kodi yangu ya flemu ni Sh 840,000 kwa mwezi na nimelipa kodi ya miezi 12 ambayo ni Sh10.8 milioni, sasa ukinipa miezi miwili ili nikupishe katika jengo lako, hiyo kodi ya miezi mingine itakuwaje?” alihoji Maleko.

Akizungumzia pendekezo la mmiliki huyo kuwapa miezi miwili, mmoja wa wapangaji, David Mwandete amesema hawajaukubali, bali wanataka aheshimu mikataba ya wapangaji.

Kwa upande wake, Jenipher Shoo amedai kuwa iwapo mmiliki huyo atashindwa kukubaliana na wapangaji wake kwa kuwaruhusu wamalize mkataba wao, basi wataliomba baraza hilo liwaandikie barua ili waende mbele kwa ajili ya hatua nyingine.