Masharti ya wenye nyumba, unayachukuliaje!
Nyumba
Muktasari:
Ukweli ukoje?
Siku zote anayetoa sharti huwa na dhamira moyoni mwake. Hudhamiria katika jambo fulani, hivyo ndivyo inavyokuwa kwa wamiliki wengi wa nyumba. Masharti mengi yatolewayo huwa ni magumu kwa wapangaji, lakini wenye nyumba wengi hufikiria kuzilinda nyumba zao zisiharibike haraka na wengine ni kulinda ustaarabu na nidhamu kwenye mazingira yao. Idadi ndogo ya wenye nyumba huwa kero kwa wapangaji kulingana na usumbufu na kuweka masharti yasiyo na malengo wala manufaa yoyote kwao na wapangaji wao
Sitaki mpangaji mwenye watoto zaidi ya wawili, mgeni akikutembelea mwisho siku tatu aondoke., sihitaji wapangaji waliiooa. Hayo ni baadhi ya masharti yenye kukera yatolewayo na wenye nyumba wengi mijini.
Lakini tujiulize chanzo cha haya yote ni nini?
Wengi wetu hutamani kumiliki nyumba, lakini kwa kuwa uwezo wa kugharamia ujenzi ni mgumu kidogo, hulazimika kupanga na hayo ndiyo tunayokumbana nayo kila siku.
Swali la wiki hii liliuliza: Umeshawahi kupewa masharti mengi na mwenye nyumba wako? Ni yapi hayo na unahisi tatizo ni nini?
Wadau wa safu hii walijibu hivi:
Issa Khatibu, Dar es Salaam
Nimewahi kupewa masharti mengi na mwenye nyumba mfano; Nisichelewe kurudi usiku, kulipa kodi ya mwaka, kupiga deki chooni kama sitaki nioe, kutokubandika makaratasi ukutani na kupiga rangi katika chumba. Tatizo hapa ni uelewa wa wamiliki wa nyumba ni mdogo na wagumu kuelewa.
Lucas Lawrence, Arusha
Niliwahi kupewa masharti mengi, aliniambia nisipambe ndani kwangu kwa sababu tunaharibu kuta na ni lazima ninunue maji ndoo moja Sh100 ya kutumia, ninunue kwake kila siku na si nje na hapo nyumbani kwake.
Muddy Guy, Gongo la Mboto
Kuna matatizo mengi sana ya wenye nyumba, wengine wanapandisha kodi kila baada ya miezi sita, ili akukomoe uhame alete mpangaji mwingine, huu si ustaarabu hata kidogo, tusinyanyase wapangaji, wote tungekuwa na nyumba nani angepanga?
Balozi Wasaku, Kigoma
Nimewahi kupewa masharti mengi tu, ambayo nimepewa na wenye nyumba ila kwa leo nitataja moja tu. Niliambiwa nisiwe nafungulia sub woofer niliyoinunua kwa bei kubwa, mi nadhani ni wivu tu kwa kuwa yeye hana.
Jenny Abbas, Arusha
Niliwahi kupanga nyumba nikiwa Dar es Salaam, wakati huo nilikuwa nafanya kazi kwa mkataba mfupi kwani kwetu ni Arusha, nilipotembelewa na rafiki zangu wa kiume wanne, walishinda, wakala, wakanywa, nilisingiziwa na mwenye nyumba kuwa nililala nao wote wanne, alinipa masharti magumu ya kutoingiza mtu yoyote, awe mwanamume au mwanamke, palinishinda nikahama.
Athuman Muya, Dar es Salaam
Nimeishi nyumba mbili tofauti, sijawahi kupewa masharti kabisa, nahisi ni kwa kuwa nilikuwa bachala.
Shebby Sheka, Dar es Salaam
Aliniambia nisiwe na watu wengi wanaonitembelea, hasa wakija wanawake ndiyo linakuwa tatizo, yaani ni balaa hadi kikao unakaliwa. Nahisi ni wivu, pali ni shinda nikahama.
Omary Ally, Zanzibar
Miaka mitano iliyopita nilipanga nyumba moja Dar es Salaam, nilioa mke nikazaa naye mtoto mmoja, aliposhika ujauzito wa mtoto wa pili, mwenye nyumba alinipa onyo na kunitaka niishie huyo huyo kwani hahitaji mpangaji mwenye watoto wengi. Aliposhika ujauzito wa tatu alinitimua, nikahama.
Swali la wiki ijayo
Mtoto anapomtukana mtu mzima mbele ya mzazi na mzazi anamwacha tu, hii ni ishara gani? Umeshawahi kutukanwa na mtoto au kuambiwa maneno ya dharau? unadhani tatizo ni nini?
Tuma maoni yako kupitia namba 0762499991 au [email protected]