Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

EU, AFD kufadhili mradi wa maji Mwanza wa Sh37 bilioni

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau (katikati), na Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Jean François (kulia), wakisaini makubaliano ya utoaji wa ruzuku ya Euro milioni 12.5 kwa ajili ya kugharamia awamu ya pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria (LVWATSAN II) jijini Mwanza.

Muktasari:

  • Mradi huo unatarajiwa kupanua huduma ya maji kwa zaidi ya watu 400,000 katika maeneo ya Mwanza Kusini, pamoja na kuboresha huduma za usafi wa mazingira.

Mwanza. Umoja wa Ulaya (EU) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) umesaini makubaliano ya utoaji wa ruzuku ya Euro milioni 12.5, sawa na takribani Sh37 bilioni kwa ajili ya kugharamia awamu ya pili ya mradi wa maji na usafi wa mazingira wa Ziwa Victoria (LVWATSAN II) jijini Mwanza.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Ijumaa Juni 19, 2026 katika chanzo na kituo cha kutibu maji cha Butimba, ikiwa ni mwaka mmoja tangu uzinduzi wa kituo hicho kinachozalisha mita za ujazo 44,000 za maji safi kwa siku.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kanda wa AFD, Jean François amesema makubaliano hayo yanaashiria zaidi ya msaada wa kifedha, bali ni uthibitisho wa dhamira ya muda mrefu ya 'Team Europe' kuboresha maisha ya wananchi wa Mwanza.

“Tunajua bado kuna changamoto za maji na usafi wa mazingira na ndiyo maana tunaendelea na uwekezaji huu mkubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mpango wa LVWATSAN II unakadiriwa kugharimu Euro milioni 202.5 (zaidi ya Sh600 bilioni), ukihusisha pia mikopo nafuu kutoka AFD na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).

Muonekano wa Kituo cha Kutibu Maji cha Butimba, kinachohudumia zaidi ya wakazi 400,000 katika maeneo ya Mwanza Kusini.

Mradi huo unatarajiwa kupanua huduma ya maji kwa zaidi ya watu 400,000 katika maeneo ya Mwanza Kusini, pamoja na kuboresha huduma za usafi wa mazingira.

Aidha, mradi huo utaanzisha mifumo rahisi ya majitaka katika baadhi ya maeneo ya Mwanza, pamoja na kuanzisha mfumo wa kisasa wa majitaka katika mji wa Bukoba kwa mara ya kwanza, utakaohudumia zaidi ya watu 100,000 huku mtandao uliopo Musoma ukipanuliwa.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau amesema ushirikiano kati ya Tanzania na EU umeendelea kuimarika kwa zaidi ya miaka 50, ukiwezesha uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, nishati na maendeleo ya miji.

Amesema EU imekuwa mshirika wa muda mrefu katika maendeleo ya sekta ya maji Mwanza kwa zaidi ya miaka 20, ikiwa ni pamoja na kufadhili miundombinu ya maji na usafi wa mazingira kwa lengo la kulinda Ziwa Victoria dhidi ya uchafuzi.

“Leo tunaendeleza dhamira yetu ya kusaidia mahitaji yanayoongezeka ya maji kutokana na ukuaji wa kasi wa Jiji la Mwanza, huku tukizingatia pia ulinzi wa mazingira,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa  Wizara ya Maji, Charles Mafie ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya LVWATSAN iliyogharimu Euro milioni 136, imefanikiwa kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika Jiji la Mwanza, Ilemela na miji ya pembezoni ikiwemo Magu, Misungwi na Lamadi, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Butimba.

Amesema miradi hiyo imenufaisha zaidi ya watu 150,000 kupitia huduma za usafi wa mazingira, huku kazi zinazoendelea zikilenga kuwafikia zaidi ya watu 450,000 kupitia upanuzi wa miundombinu ya maji.

"Kupitia awamu ya pili, uzalishaji wa maji unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia lita milioni 170 kwa siku, sambamba na ujenzi wa mitandao mipya ya mabomba yenye urefu wa takribani kilomita 700 na matumizi ya nishati ya jua ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa uhakika zaidi,"amesema.

Ameeleza mradi huo pia unatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 750,000 wanaoishi katika maeneo ya Mwanza Kusini kwa kuwapatia maji safi na salama saa 24.

Amesema Serikali inathamini mchango wa washirika wa maendeleo, akisisitiza kuwa uwekezaji huo unaendelea kuboresha maisha ya wananchi na kukuza maendeleo endelevu nchini.

Katika hatua nyingi EU na AFD imetembelea na kukagua mfumo wa maji taka uliopo wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.