Mkama Bwire bosi mpya Dawasa
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkama Bwire
Dar es Salaam. Leo Jumatano, Julai 3, 2024, Mkama Bwire ameteuliwa kushika nafasi ya Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) katika kikao maalumu cha Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Bodi ya Wakurugenzi Dawasa.
Kikao hicho kimefanyikia ofisi za Dawasa, Ubungo jijini Dar es Salaam. Bwire ni Mtumishi wa Wizara ya Maji ambaye amehudumu kama Mhandisi wa Maji katika Halmashauri ya Kibaha, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tabora (Tuwasa).
Hadi anapokea jukumu hilo alikuwa ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini katika Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa). Anachukua nafasi ya Kiula Kingu, aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo na kuwekwa kando Juni 30, 2024 na kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za uhaba wa upatianaji wa maji.
Kingu alisimamishwa pamoja na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Huduma ya Maji, Shaban Mkwanywe. Wengine Meneja wa Dawasa-Kinyerezi, Burton Mwalupaso, Mhandisi wa Kibamba, Regan Masami na kumuondoa kwenye nafasi yake Meneja wa Dawasa-Kibamba Elizabeth Senkele wote kwa makosa ya kushindwa kuwajibika.
Wote hao wamesimamishwa kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Waziri Aweso na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kujionea hali ya upatikanaji wa huduma hiyo.