Mke wa mshtakiwa kesi ya kina Mbowe aeleza mtuhumiwa alivyowekwa kabatini

Mke wa mshtakiwa kesi ya kina Mbowe aeleza mtuhumiwa alivyowekwa kabatini

Muktasari:

  •  Lilian Kibona,  shahidi wa tatu wa upande wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amedai mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo aliwekwa kabatini akiwa mahabusu ya Segerea.



Dar es Salaam. Lilian Kibona,  shahidi wa tatu wa upande wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amedai mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo aliwekwa kabatini akiwa mahabusu ya Segerea.

Kibona ambaye ni mke wa mshtakiwa wa pili katika kesi ya ugaidi, Adamu Kasekwa ametoa madai hayo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mustapha Siyani.

Akitoa ushahidi wake leo Jumatano Septemba 29, 2021 mahakamani hapo shahidi huyo ameeleza jinsi yeye na wake wa washtakiwa wengine walivyozunguka katika vituo mbalimbali vya polisi na hospitali  Agosti 13, 2020 kumtafuta mumewe na wenzake, baada ya kumkosa katika simu wakati huo mumewe huyo alikuwa amekwenda Moshi na wenzake.

Amedai  baada ya kuwakosa kote waliamua kukaa tu hadi alipoona katika taarifa ya habari kupitia kituo cha televisheni cha ITV, walipofikishwa mahakamani Agosti 19, 2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Amedai katika taarifa hiyo ya saa 2 usiku ilieleza kuwa washtakiwa walipelekwa mahabusu lakini haikujulikana kuwa walipelekwa katika mahabusu gani.

Amedai kwa kuwa yeye alikuwa nyumbani kwake Chalinze, aliwasiliana na wake wa washtakia wengine ambao ni rafiki za mumewe, ambao walikwenda kuwatafuta na hatimaye kumkuta mumewe, Kasekwa na mwenzake Ling'wenya katika mahabusu ya Segerea.

Amedai siku alipokwenda kumuona baada ya kujitambulisha kwa askari aliyewapokea alipotaja jina la mumewe, alimsikia mmoja wa askari Magereza akisema kuwa ndiye yule aliyewekwa kabatini.

"Nilikwenda kumuona mahabusu Jumamosi. Nilipojitambulisha na kumtaja jina lake, niliwasikia askari wenyewe wakisema ndio yule jamaa ambaye yuko kabatini," amedai shahidi huyo.

Amedai  baada ya hapo askari walichukua funguo wakasema wanakwenda kumleta na wakamtaka asubiri mahali pale alipokuwa.

Shahidi huyo amedai kuwa, Kasekwa aliletwa mbele yake na kwamba alimuona hali yake ikiwa imebadilika sana kwa kuwa alikuwa akitembea kwa kuchechemea, akiwa amekonda huku macho yakiwa yameingia ndani na akiwa makovu mkononi ambayo wakati anaondoka hakuwa nayo.

"Nilimuuliza hali yake na kilichotokea akasema kuwa hali yake ni hivyo hivyo lakini siyo nzuri. Aliniambia kuna mateso alipilitia akiwa Moshi. Amesema nilipigwa sana ndio maana unaona niko katika hali hii," amedai shahidi.