Mbowe anavyojifariji kwa kitabu hiki mahabusu

Mbowe anavyojifariji kwa kitabu hiki mahabusu

Muktasari:

  • Norman Vincent Peale, alikuwa mwanathilojia na mhubiri wa Injili aliyetimiza wajibu wake ipasavyo Karne ya 20. Desemba 24, 1993, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 95. Hakufa na kuondoka, bali aliacha fikra zinazoishi.


Dar es Salaam. Norman Vincent Peale, alikuwa mwanathilojia na mhubiri wa Injili aliyetimiza wajibu wake ipasavyo Karne ya 20. Desemba 24, 1993, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 95. Hakufa na kuondoka, bali aliacha fikra zinazoishi.

Ni fikra hizo ndizo zinamfanya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ajipambanue nazo, akitaka jumuiya ya Watanzania na duniani kote kuamini kwamba yupo imara na hatafsiri kilichopo kwa chuki. Hapa najaribu kucheza na ubongo wa Mbowe kwa lugha ya picha.

Mwaka 1952, Peale alitoa kitabu kinachoitwa “The Power of Positive Thinking” – “Nguvu ya Fikra Chanya”.

Shabaha iliyopo kwenye maudhui ya kitabu hicho ni kuwajenga watu kuishinda mitazamo ya hofu na kuwaelekeza kuwa na imani isiyotetereka, kwamba Mungu yupo na ndiye mwenye udhibiti wa mwisho katika kila nyakati.

“The Power of Positive Thinking” kilichapwa miaka tisa kabla Mbowe hajazaliwa. Amekua na kukisoma.

Bila shaka anakiamini. Anazithamini fikra za Peale. Kipindi hiki akiwa mahabusu na safari nyingi za mahakamani, akikabiliwa na mashitaka ya ugaidi, mara nyingi hupigwa picha akiwa ameshikilia kitabu hicho; Nguvu ya Fikra Chanya!

Mbowe, huingia na kitabu hicho mahakamani na hutoka nacho. Utamuona akikiweka vizuri ili wanahabari na wapigapicha wakichukue na maandishi ya kwenye jalada yasomeke.

Anapokaribia basi la magereza tayari kwa safari ya kuendelea na maisha ya mahabusu, hukiweka kitabu hicho kwapani, mkono mmoja akisalimia wafuasi wake kwa alama ya “vema” (salamu ya Chadema), kisha huingia garini.

Tuchambue lugha ya picha; kitabu cha “The Power of Positive Thinking”, Peale anaanza sura ya kwanza kwa kueleza kanuni 10 za kukabili mitazamo ya hofu na kubaki mwenye imani na Mungu. Namba moja anasema, “Jijengee picha ya kushinda kila siku”. Kwamba mitihani ya dunia na hofu, visikufanye upoteze ari ya ushindi.

Kanuni ya pili ni “Fikiri kwa fikra chanya hadi fikra hasi zitoweke”. tatu ni “Kupunguza vikwazo”, nne “Usijaribu kuiga wengine”, tano “Rudia maneno ‘kama Mungu yupo nasi, nani anaweza kushindana basi?’ rudia maneno hayo mara 10 kila siku.”

Katika kanuni ya sita, Peale anafundisha, “Kufanya kazi na mshauri”, saba “Rudia maneno ‘naweza kufanya yote kupitia Yesu ambaye ananifanya niwe imara’ mara 10 kila siku.” Nane “Imarisha heshima yako binafsi.” Tisa, “Weka mkazo kwamba upo kwenye mikono ya Mungu.” 10 “Amini kuwa unapokea nguvu kutoka kwa Mungu.”

Sura ya pili, Peale anaainisha umuhimu wa kujitengenezea fikra zenye amani kwa kusoma maandishi yenye kujenga moyo, kusikiliza na kutazama mambo yanayosafisha fikra.

Sura ya tatu, ni elimu kuhusu jinsi ya kuwa na nguvu isiyoyumba. Aliandika “Mungu ni chanzo cha kila nishati”. Alifafanua kuwa ubongo hudhibiti hisia zote za mwili. Ukiacha nishati na hisia hasi viondoke, utaingiza vilivyo chanya kupitia Mungu.

Sura ya Nne, Peale anazungumzia nguvu ya uponyaji kupitia maombi, jinsi unavyoweza kupona maumivu ya mwili na hisia kwa sala, kisha kuweza kunyanyuka kutoka kwenye mitihani mbalimbali ya kidunia.

Peale anaelekeza watu kubaki upande wa Mungu na kusali sana kipindi wakiwa katika masaibu ya ulimwengu.

Sura ya tano na sita, Peale anafundisha kuwa furaha hutengenezwa kwa uchaguzi binafsi. Kwamba ni wewe mwenyewe utaamua maisha yako yawe na furaha au majonzi. Zaidi, anakataza hofu, mwa maana ni kizuizi cha furaha.

Inaelekezwa katika sura ya saba kwamba hatua muhimu ya kuwa na fikra chanya ni siku zote kuamini katika kushinda. Imani ya kushindwa inapigwa marufuku, kwani vikwazo vingi hutengenezwa akilini.

Sura ya nane mpaka 11, Peale anajenga hamasa ya kifikra kwamba watu wajitenge na woga wa kimazoea. Anafafanua kuwa mtu aliyejijengea tabia ya hofu, hujiwekea vikwazo vya kimaisha. Ukiweza kudhibiti hofu, utasafisha fikra na kujiimarisha kwa namna chanya.

Zaidi, Peale anakumbusha watu kuomba msaada wa Mungu, kwani ndiye mwenye uwezo wa juu wa kutatua matatizo yote na kuponya maumivu yenye kuonekana na ya hisia.

Anashauri binadamu kutosahau uwepo wa Mungu hasa wanapokuwa kwenye nyakati nguvu zilizosheheni majaribu.

Sura ya 12, Peale anaeleza kuwa kuruhusu hasira ziondoke na kukumbatia hali ya utulivu inaweza kukusaidia hata katika maradhi ya mwili, kama ukurutu. Sura ya 13, anafundisha jinsi ambavyo ukiruhusu fikra chanya kuingia ndani yako, inavyoweza kubadilisha mwonekano wako wa nje wa kimaisha. Sura ya 24, anasema, ukijituliza kwa Mungu bila wasiwasi utaishi maisha yenye kutosheleza.