Boaz, Kingai kizimbani kesi ya Mbowe
Muktasari:
- Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa Rushwa na Uhujumu Uchumi leo itaanza kupokea ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Jumatano Septemba 15, 2021 itaanza kupokea ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Mashahidi hao ni pamoja na maofisa wa Jeshi la Polisi, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai.
Wengine ni maofisa wa Polisi kutoka makao makuu ya jeshi hilo vitengo vya makosa ya kimtandao, uchunguzi wa silaha na uchunguzi wa maandishi na wengine kutoka mikoani.
Mashahidi wengine ni maaskari kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), akiwamo Luteni Denis Leo Urio kutoka Kikosi cha Jeshi cha Makomandoo, 92 KJ Ngerengere, mkoani Morogoro.
Pia wamo maofisa wa sheria kutoka kampuni za huduma za simu za mkononi za Mic Tanzania Ltd (Tigo) na Airtel.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.