Mabalozi waonywa kesi ya Mbowe

Mabalozi waonywa kesi ya Mbowe

Muktasari:

  • Balozi Mulamula asema mabalozi wanaokwenda mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ya Mbowe wanapaswa kufuata sheria

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewataka mabalozi wanaokwenda Mahakamani kufuatilia mwenendo ya kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufuata sheria na taratibu za kidiplomasia.

Balozi Mulamula alisema hayo jijini hapa juzi, alipozungumza na mabalozi, wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa kuhusu mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) uliofanyika Lilongwe, Malawi Agosti 17 – 18.

Katika mkutano huo, Balozi Mulamula alisisitiza mabalozi wanaokwenda mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ya Mbowe kufuata sheria na taratibu za kimataifa za kidiplomasia ili kujiepusha na ukiukwaji wa sheria na taratibu hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mulamula alisema Serikali haina lengo la kuwazuia mabalozi hao kwenda mahakamani kufuatilia kesi hiyo, lakini kutokana na na uwepo wa janga la Uviko-19 pamoja na msongamano, ni muhimu kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufuatilia shauri hilo kwa njia nyingine, ikiwamo kupitia vyombo vya habari.

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndio yenye jukumu la kuhakikisha usalama wa wanadiplomasia waliopo hapa nchini.

Hata hivyo, kwa siku za hivi karibuni baadhi ya wanadiplomasia hao wameonekana mahakamani bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya kidiplomasia, ikiwamo kutoa taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema Balozi Mulamula katika taarifa hiyo.

Kiongozi wa mabalozi waliopo hapa nchini, Dk Ahamada El Badaoui alisema ulinzi wa mabalozi waliopo hapa nchini ni muhimu na endapo kuna mabalozi wanafanya hivyo ni vyema wakafuata taratibu na sheria zilizopo.

Akizungumza na gazeti hili, mjumbe wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, alisema wamepokea tahadhari kutoka serikalini kwa wanadiplomasia na kwamba serikali inatathmini hali ya usalama wao.

“Tulihudhuria usikilizwaji wa kesi inayomkabili kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema, Freeman Mbowe kwa sababu ni haki yetu kama mabalozi kufuatilia hali ya kisiasa katika nchi ambayo tumo wakati huo,” alisema mjumbe wa EU.