Rais Samia azungumzia kesi ya Mbowe

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akisema, uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ulianza Septemba mwaka jana, lakini ulikuwa haujakamilika, amefafanua kuwa mashtaka yake hayakuchochewa kwa sababu za kisiasa.

Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akisema, uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ulianza Septemba mwaka jana, lakini ulikuwa haujakamilika, amefafanua kuwa mashtaka yake hayakuchochewa kwa sababu za kisiasa.

Mkuu huyo wa nchi alisema anachojua ni kuwa Mbowe alifunguliwa kesi Septemba mwaka jana, akiwa na wengine kwa mashtaka ya ugaidi na uhujumu uchumi.

Hata hivyo, alisema kwa wenzake kesi zao zilishaanza kusikilizwa, lakini Mbowe upelelezi wake ulikuwa haujaisha.

Rais Samia alieleza hayo kwa mara kwanza katika mahojiano na Shirika la Utangaza la Uingereza (BBC), yaliyoongozwa na mtangazaji mwandamizi wa kituo hicho, Salim Kikeke kutoka Ikulu, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

“Tumeingia kwenye uchaguzi, tumemaliza. Sasa polisi wamemaliza uchunguzi wao wamemhitaji kwa ajili ya kuendelea na kazi yao. Lakini kama utakumbuka Mbowe hakuwa nchini kwa kipindi kirefu, alikuwa Nairobi.

“Lakini alivyoingia nchini aliitisha maandamano ya Katiba. Nadhani yalikuwa na mahesabu akijua kuwa ana kesi ya namna hiyo na hii vurugu anayoianzisha, akikamatwa aseme kwa sababu ya Katiba,” alieleza Rais Samia.

Samia alisema suala la Mbowe lipo mahakamani hana uhuru wa kulizungumzia kwa kina, huku akishauri jambo hilo liachwe katika chombo hicho cha kutenda haki ili kifanye kazi yake na kuuonyesha ulimwengu kama shutuma za Mbowe za kweli au la.

Agosti 6 mwaka huu, Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) na wenzake watatu walisomewa mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo hivyo.

Mashtaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria. Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.

Kukutana na vyama

Kuhusu kukutana na viongozi wa vyama siasa, Rais Samia alisema; “Nilitaka kukutana nao, lakini si wakiwa wamechambukachambuka, kwa sababu hawa wana vyama vyao vidogo vidogo na mabaraza yao. Nilitaka kwanza wajiunde kwenye baraza lao ambalo lilifanya uchaguzi wiki chache zilizopita.”

Alisema kwa vile wameshafanya uchaguzi na kamati zao ndogo zimejiunda vizuri, atatafuta siku ya kuzungumza nao.

Alisema hata yeye anataka kuzungumza nao ili kuwaeleza mwelekeo wake baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2020 kwa kuwa katika harakati za kujenga nchi hachagui; akimuona mpinzani ana mwelekeo mzuri atamweka katika Serikali ili kujenga Taifa. Alibainisha kuwa hakuna sehemu yoyote inayoeleza kuwa baada ya uchaguzi, chama kilichoshinda ndicho kitakachojenga nchi peke yake.

“Mtanzania yeyote mwenye mtazamo mzuri wa kisiasa, anayeweza kutimiza majukumu yake na kuleta yale wananchi wanayoyahitaji, namtumia tu. Namwingiza kwenye mfumo wangu, twende. Nataka waje tukae tuone tunakwendaje na hili,” alisema Rais Samia.