Kesi ya Mbowe ngoma nzito Kisutu

Mbowe, wenzake wafikishwa Kisutu

Muktasari:

  • Unaweza kusema ni ngoma nzito. Teknolojia ya video iliyopangwa kutumika katika usikilizaji wa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu jana ilishindikana.

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni ngoma nzito. Teknolojia ya video iliyopangwa kutumika katika usikilizaji wa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu jana ilishindikana.

Hatua hiyo sasa itakuwa fursa kwa mamia ya wafuasi wa chama hicho waliofika katika Mahakama ya Kisutu kumuona kiongozi wao, kukata kiu yao atakapofika kortini leo.

Jana, licha ya kuwapo zuio na ulinzi mkali wa polisi mashabiki hao walifanikiwa kujaa nje ya mahakaman hiyo, japo baadhi yao waliishia mikononi mwa polisi.

Kushindikana kwa teknolojia hiyo, kuliifanya mahakama hiyo kutoa hati ya kuwaita washtakiwa hao mahakamani, ili waweze kusikiliza kesi yao.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kutenda kosa na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Mbali na Mbowe, katika kesi hiyo ambayo Ubalozi wa Canada nchini ulieleza kuwa unaifuatilia kwa ukaribu, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, ubalozi huo ulisema: “Demokrasia yenye nguvu inahitaji mfumo wa haki na uwazi kwa raia wote; uhuru wa kujieleza na kukusanyika; na vyombo vya dola vinavyozingatia haki za binadamu na kuhakikisha usalama kwa raia wote.

Jana kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa kubadilisha hati ya mashtaka, lakini ilishindwa kuendelea kwa njia ya video, baada ya kutokea hitilafu katika mtandao hadi Mahakama ya Kisutu ikashindwa kuwasiliana na Gereza la Keko waliko washtakiwa.

Awali, mawakili wa Serikali Pius Hilla, Christopher Msigwa na Grace Mwanga waliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa imeitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba.

Wakipokezana, walidai kuwa mara ya mwisho kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo, hati ya mashtaka iliwasilishwa na hivyo waliomba kuwasomea upya mashtaka washtakiwa hao.

Wakati Hilla akieleza hayo, washtakiwa walidai hawaoni kinachoendelea mahakamani hapo bali wanasikia tu sauti.

Mbowe akiwa gerezani alionekana akiwa amevalia fulana nyeupe yenye mistari myeusi na suruali ya jinsi rangi ya bluu.

Kutokana na hitilafu ya washtakiwa kushindwa kuona kinachoendelea mahakamani, mtaalamu wa Tehama alijaribu kurekebisha mitambo na iliposhindikana Hakimu akakubaliana na mawakili wa pande zote kesi hiyo iahirishwe hadi leo itakapotajwa.

“Kutokana na teknolojia ya video conference kupata matatizo, tumekubaliana shauri hili tuahirishe hadi kesho (leo) kwa ajili ya taratibu nyingine na ninatoa hati ya kuwaleta washtakiwa mahakamani hapa ili waweze kusikiliza kesi yao,” alisema Simba.

Leo Ijumaa, Agosti 6, 2021 muda wa 2:12 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kukiwa na ulinzi mkali.

Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani hapo saa leo Ijumaa, Agosti 6, 2021 muda wa 2:12 wakiwa kwenye basi dogo la Magereza likisindikizwa na magari mawili ya wazi yenye askari magereza wenye silaha za moto.

Baada ya kuwasili washtakiwa wote walishuka na kuelekea kwenye mahabusu ya Mahakama.