Corona yaua 29 Tanzania huku wagonjwa 176 wakipatikana kwa siku moja

Muktasari:

Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima amesema hadi sasa jumla ya watu 29 wamefariki kutokana na wimbi la tatu la Covid-19 huku jana pekee kukiwa na wagonjwa wapya 176.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima amesema hadi sasa jumla ya watu 29 wamefariki kutokana na wimbi la tatu la Covid-19 huku jana pekee kukiwa na wagonjwa wapya 176.

Idadi hiyo inafikisha Tanzania kuwa na jumla ya wagonjwa 858 wa Covid-19.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dk Dorothy amesema takwimu hizo ni alizopata jana hivyo upo uwezekano vifo zaidi vikawa vimetokea.

Waziri ameeleza kuwa licha ya Serikali kuendelea kusisitiza  watu kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo bado wapo wanaozembea.

“Itoshe kuwaambia kuwa ugonjwa upo na watu wanakufa, tusingependa kupeana hizi taarifa za vifo tuchukue tahadhari, kila mmoja wetu ajiulize unapofanya mambo kinyume na kuchukuta tahadhari unalenga kumtesa nani,” amesema Dk Gwajima.

Waziri huyo pia alitupa lawama kwa  viongozi wa Serikali ambao hawashiriki kwenye vita vya kupambana na ugonjwa huo.

“Nawakumbusha watu hawa wasiotaka kwenda mstari wa mbele wasichukulie mzaha Uviko 19, ugonjwa huu upo tusijiachie kwa sababu wimbi la kwanza na la pili lilipita,”.