Kesi ya Mbowe yaibua mapya

Kesi ya Mbowe yaibua mapya

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mbalimbali yakiwamo ya ugaidi, sasa wameigeukia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kuhusiana na kesi yao hiyo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mbalimbali yakiwamo ya ugaidi, sasa wameigeukia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kuhusiana na kesi yao hiyo.

Mbowe na wenzake wanadai kuwa, kwa kauli hiyo ambayo Rais aliitoa alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Agosti 9, 2021, imeingilia uhuru wa Mahakama na kwamba kwa hali hiyo usikilizwaji wa kesi yao hautakuwa wa haki na usawa.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliozungumza na Mwananchi kuhusiana na kile alichokisema Rais Samia katika mahojiano hao, walieleza kuwa hawaoni kama kuna namna ambayo Rais ameingilia uhuru wa Mahakama.

Mbowe na wenzake hao wanakabiliwa na kesi hiyo ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako imefunguliwa kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali, kabla ya kupelekwa Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo.

Katika mahojiano yake na BBC, akijibu swali la mtangazaji Salim Kikeke kuwa wafuasi wa Mbowe wanadai kuwa kesi hiyo ya ugaidi dhidi ya Mbowe ni ya kisiasa, Rais Samia alikanusha kuwa si ya kisiasa na kwamba mashtaka hayo yalikuwepo tangu Septemba 2020.

Hata hivyo, Rais Samia alisema kuwa kwa kuwa suala hilo bado liko mahakamani hawezi kusema sana na kwamba mahakama ndio itakayoamua na kuieleza dunia kama tuhuma za Mbowe ni za kweli au si za kweli.

Wakati kesi hiyo ilipoitwa mahakamani hapo juzi kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya kesi (maelezo ya mashahidi na vielelezo) washtakiwa hawakuwepo mahakamani kwa kile kilichoelezwa kuwa ni tatizo la usafiri, baada ya gari la Magereza kupata hitilafu hivyo kesi yao ikaendeshwa njia ya mtandao.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wao, Peter Kibatala aliieleza mahakama hiyo kuwa wameshawasilisha mahakamani hapo taarifa kuna masuala yameibuka katika kesi hiyo yanayohusu ukiukwaji wa Katiba.

Kwa mujibu wa wakili huyo, Mbowe na wenzake wanadai kuwa katika mahojiano hayo, Rais alitoa taarifa ambazo si za kweli na kwamba pia zinakwenda kwenye kiini cha shauri ambalo bado liko mahakamani na halijaamriwa.

Wanadai kuwa kuwa kauli hiyo ya Rais iliripotiwa katika vyombo vya habari na kutolewa maoni mbalimbali, ambayo yanaonyesha taswira ya washtakiwa kuwa ni kweli wana hatia mbele ya jamii.


Mbowe anyoosha mkono

Wakati mjadala huo ukiendelea baina ya mawakili wa upande wa mashtaka na ule utetezi, mshtakiwa Mbowe alinyoosha mkono juu akiwa gerezani na alipopewa nafasi ya kuongea, alidai kuwa hasikii kile ambacho kinaelezwa mahakamani hapo na kuomba kuletwa mahakamani hapo.

Walichosema wanasheria

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Wakili Francis Stolla alilieleza kuwa kwa namna alivyozungumza Rais Samia kwa maoni yake, haoni kama ameingilia uhuru wa Mahakama.

“Kwa kuwa alisema kuwa tuiche mahakama ifanye kazi yake na iamue kama wana tuhuma zao ni za kweli au la, nadhani hiyo ndiyo namna ya kiungwana kwa mtu anayeabudu utawala wa sheria,” alisema Wakili Stolla.

Naye Wakili Ibrahimu Bendera alisema kuwa ingawa hajui kama kweli ni kesi ya kisiasa kama wafuasi wa Mbowe wanavyodai, lakini alisema kuwa kauli hiyo ingeweza kuwa imeingilia uhuru wa Mahakama, kama angekuwa ametoa amri ya kuelekeza matokeo.

Mbali na Mbowe, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo namba 63 ya mwaka 2020, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamo, Mohamed Abdillahi Linngwenya.

Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo, aliahirisha hadi Agosti 27 kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi hayo ya kupelekea masuala hayo yanayolalamikiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya uamuzi.