Chadema kupinga kesi ya Mbowe

Chadema kupinga kesi ya Mbowe

Muktasari:

  • Wakati Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akitangaza kuwa wanakusudia kufungua kesi kupinga kukamatwa na kushtakiwa kwa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kutetea kukamatwa kwa kiongozi huyo, kikisema askari waliomkamata walifuata matakwa ya kisheria.

Dar es Salaam. Wakati Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akitangaza kuwa wanakusudia kufungua kesi kupinga kukamatwa na kushtakiwa kwa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kutetea kukamatwa kwa kiongozi huyo, kikisema askari waliomkamata walifuata matakwa ya kisheria.

Julai 21, Mbowe alikamatwa jijini Mwanza alipokwenda kuhudhuria kongamano la Katiba mpya lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), kisha kusafirishwa hadi jijini Dar es Salam, ambapo baadaye alipandishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa yanayohusu ugaidi.

Akizungumza na wanahabari juzi, Mnyika alisema, baada ya mwenyekiti huyo kukamatwa, Kamati Kuu ilikutana Julai 22, 24 na 28 ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu anayeishi nchini Ubelgiji na kujadili hatua za kufuatwa na chama hicho.

“Kamati Kuu imeelekeza mawakili wa chama kufungua shauri la kikatiba kupinga ukiukwaji wa haki za kisheria na tayari utekelezaji huo umeanza,” alisema Mnyika.

“Kamati kuu imefikia uamuzi huu baada ya kupitia hati ya mashtaka aliyofunguliwa na baada ya kuipitia tumebaini haina mashiko ya kisheria,” aliongeza.

Aidha, Mnyika alisema Kamati Kuu imeelekeza Agosti 5 wakati kesi hiyo ikitajwa, iwe ni siku ya kuendeleza mapambano ya kudai Katiba mpya.

“Chadema inatoa wito kwa watu wote ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam, siku hiyo kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia mwenendo wa kesi hii,” alisema.

Alibainisha kuwa baada ya kufuatilia kwa kwa kina, wamebaini mashitaka hayo yametumika kama nyenzo ili kukosa uhuru wa kuendesha operesheni ya kudai Katiba mpya. Mnyika amewataka viongozi wa chama hicho pamoja na wanachama wote kujadili na kuendeleza mapambano ya kudai Katiba mpya.

Hata hivyo, hivi karibuni wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kwa sasa kipaumbele ni kujenga uchumi wa nchi ambao umeshuka kutokana na janga la corona.

Kauli hiyo ya Rais Samia ni ya pili kuitoa tangu alipoingia madarakani ambapo mara ya kwanza aliitoa wakati akiwaapisha mawaziri katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Katika hafla hiyo Rais Samia alisema: Hili la Katiba mpya naomba lisubiri kidogo.”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro alisema shauri linalomkabili Mbowe liko mahakamani hakuna mtu au kikundi chochote kinachoweza kuingilia au kuitisha mahakama.

Alisema kufuatilia shauri mahakamani ni haki ya kila mtu lakini kitendo cha Mnyika kuitisha watu kuzidi uwezo wa mahakama, hakikubaliki.

“Mahakama ni chombo huru kinachofanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria, hakiwezi kutishwa na mambo aliyoyasema Mnyika, hivyo ninamtahadharisha yeye na wanachama wengine kwa kuwa Jeshi la Polisi halitawavumilia,” alisema Muliro.

Muliro alimtaka katibu mkuu huyo kama kuna jambo lolote analolilalamikia, afuate utaratibu ikiwemo vyombo vya sheria.


CCM waibuka

Akizungumza muda mfupi baada ya mkutano wa Mnyika na wanahabari, Katibu wa NEC ya CC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema si ajabu na wala si kosa kwa polisi kumkamata kiongozi yeyote wa kisiasa au wa kiserikali, ikiwa wataona kuna haja ya kufanya hivyo.

Shaka alisema kinachofanywa na Chadema ni kutapatapa, na kuuhadaa umma wa Watanzania na jumuiya za kimataifa ilhali masuala ya ndani ya nchi hufanyika bila kibali kutoka jumuiya za kimataifa.

Shaka alisema si kweli kwa mujibu wa matamshi ya Mnyika kudai Tanzania iko katika mapambano ya demokrasia wakati demokrasia ipo kisheria na kikatiba zaidi, huku Tanzania ikiwa ni nchi ya kupigiwa mfano katika kuzingatia ustawi wa haki za binadamu na demokrasia.


Ushauri kwa Chadema

Mwanasheria Timon Vitalisi alisema kesi ya kikatiba inaweza kufunguliwa endapo kuna ukiukwaji wa haki za kibinadamu na sio kupinga mashitaka.

Alisema huwezi kupinga upungufu kwenye hati ya mashtaka isipokuwa kama unafungua kesi ya kikatiba kwa ajili ya kuhoji ukiukwaji wa haki wakati wa mchakato wa kufungua shauri hilo mahakamani.

“Kesi ya kikatiba inachukua mkondo kama wa madai, ndio maana hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali huwekwa mmoja kati ya walalamikiwa, hivyo huwezi kugeuza mkondo wa jinai kuupinga kupitia mkondo wa madai,”alisema Vitalisi.

Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema Chadema ni chama cha siasa, kinapoona kinavurugwa kwa namna moja au nyingine ni lazima kitafute namna ya kuweza kujinasua kwenye huo mvurugano.

Alisema wanajaribu kujenga presha kwa Serikali na chama kinachotawala ili wagundue pengine wamewakandamiza sana.

“Kimsingi huu uhusiano wa kisiasa baina ya taasisi hizi zinazotambulika kikatiba, ambavyo ni vyama vya siasa pale chama kinapoona kinakandamizwa sana lazima kipige kelele na kuna namna nyingi za kupiga kelele na wakati mwingine hata kufanya maandamano,” alisema Dk Mbunda.


Mbowe alivyofikishwa kortini

Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili, likiwemo la kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Mbowe alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin akisaidiana na Tulimanywa Majigo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.