Freeman Mbowe aja kivingine

Freeman Mbowe aja kivingine

Muktasari:

  • Afungua kesi ya kikatiba kuishtaki Serikali, adai kutishiwa na RPC akielezwa ‘safari hii hachomoki’

Dar es Salaam. Wakati kesi ya ugaidi dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ikitajwa mahakamani kesho, kiongozi huyo amekuja kivingine akifungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu dhidi ya Serikali akipinga taratibu za kukamatwa na kushtakiwa kwake.

Miongoni mwa madai yake, Mbowe anapinga kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi kimyakimya bila kumtaarifu kwanza kuhusu mashtaka hayo pamoja na maneno ya vitisho anayodai kupewa na polisi kabla ya mashtaka hayo.

Vilevile mwanasiasa huyo anelalamikiwa haki zake kukiukwa kwa ndugu na wakili wake kutokujulishwa na kupewa fursa ya kuwasilishwa.

Mbowe anadai wakati ameshikiliwa katika kituo cha Polisi Oysterbay alikuwa akipokea kauli za kejeli na vitisho kutoka kwa ofisa wa polisi.

Pamoja na mambo mengine, Mbowe katika hati ya kiapo chake kinachounga mkono madai yake anazitaja kauli hizo anazodai kuwa zilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (RPC), aliyemtaja kwa jina Ramadhani Kingai kuwa:

“Wewe si unajifanya unaijua Katiba Mpya, safari hii huchomoki, tunakupiga kesi ya ugaidi”, inasomeka sehemu ya hati ya kiapo hicho cha Mbowe.

Mbowe alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Julai 26, 2021 na kusomewa mashtaka ya ugaidi kimyakimya katika kesi aliyoungianishwa na washtakiwa wengine waliokuwa wameshapandishwa kizimbani tangu mwaka 2020.

Alisomewa mashtaka hayo bila kuwepo mawakili, wanafamilia wala wanahabari kisha akapelewa rumande kwa kuwa mashtaka hayo hayana dhamana.

Kabla ya hatua hiyo Mbowe alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa siku tano tangu alipotiwa mbaroni Julai 21, 2021 usiku akiwa jijini Mwanza alikokwenda kwa maandalizi ya kongamano la kudai Katiba Mpya lililokuwa limeandaliwa na Baraza a Vijana wa Chadema (Bavicha).

Usiku huohuo alisafirishwa mpaka Dar es Salaam hadi nyumbani kwake ambako alifanyiwa upekuzi kisha akashikiliwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Oysterbay hadi alipopandishwa kizimbani.

Wakati akisubiri kesi yake kutajwa kesho, Ijumaa iliyopita Mbowe kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala alifungua kesi ya Kikatiba dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu.

Katika kesi hiyo namba 21 ya mwaka 2021, Mbowe anadai kuwa mdaiwa wa kwanza (DPP) na wa pili (IGP) walikiuka haki zake za kikatiba kwa kumfungulia kesi nzito ya kikatiba bila kwanza kumtaarifu kwa maandishi na kumwezesha kuwasiliana na wakili wala ndugu zake.

Hivyo, anaiomba Mahakama Kuu itoe nafuu mbalimbali ambazo ni pamoja na masharti ya lazima ya vifungu namba 131 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kupanga na Uhujumu Uchumi, Sura ya 200.

Vifungu hivyo vinatoa sharti la lazima kwa ofisa wa polisi anayemshtaki mtuhumiwa na kwa mahakama ambako mtuhumiwa anashtakiwa kumjulisha mshtakiwa kwa maandishi kuwa atashtakiwa makosa husika, lakini pia vinampa fursa ya kuwasiliana na ndugu na wakili wake kuhusiana na mashtaka hayo.

Vilevile mahakama hiyo inaombwa itamke kuwa kifungu cha 29(1) cha sheria hiyo ya uhujumu uchumi kinachotoa sharti la lazima kwa ofisa wa polisi anayemshikilia mtuhumiwa mahabusu amfikishe katika Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi ndani ya saa 48, tangu kukamatwa kwake, kilikiukwa.

Mbowe pia anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa DPP na AG walikiuka haki zake zinazotolewa na kulindwa chini ya masharti ya kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Uhujumu.

Anabainisha kuwa pamoja na mambo mengine, madai hayo yanalenge kuzuia matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya mtuhumiwa katika Kituo cha Polisi ambako mtuhumiwa anakuwa amewekwa mahabusu baada ya kutiwa mbaroni.

Anadai kuwa alipokuwa akishikiliwa mahabusu aliwekwa katika mazingira yasiyofaa, ikiwemo kulala sakafuni (bila matandiko yoyote) kuanzia Julai 21 alipokamatwa jijini Mwanza mpaka Julai 26, 2021 alipopandishwa kizimbani.

Mbowe pia anaiomba mahakama itamke kuwa DPP na IGP pamoja na Mahakama ya Kisutu, ikitenda kwa amri ya DPP na AG, walikiuka haki zake zinazolindwa na masharti kifungu cha 29 (2) na (3) cha sheria ya uhujumu uchumi kwa kushindwa kumjulisha kwa maandishi kwamba atashtakiwa kwa mashtaka mazito chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Pia anadai kwa makusudi walishindwa kumwezesha kupata fursa na njia za mawasiliano ili kuwasiliana na wakili na au ndugu zake kuhusiana na kufikishwa mahakamani Julai 26, 2021 kabla ya kufikishwa mahakamani na hatimaye akafikishwa kortini na kusomewa mashtaka bila huduma za mawakili.

“Hatimaye nilipelekwa mahakamani katika chemba ya Mheshimiwa Thomas Simba (Hakimu Mkazi Mkuu) ambako nilisomewa mashtaka hayo. Mashtaka yalikuwa mazito lakini kwa kutokuwa na mwanasheria sikufahamu maana yake,” anasema Mbowe katika kiapo chake.

Aliongeza, “Kimsingi, nikabaki kuwa mtazamaji tu wa kesi yangu mwenyewe. Sikupewa hata nakala ya hati ya mashtaka. Mahakama haikujihusisha nami kwa namna yoyote kuona kama nilikuwa na uwakilishi.

“Haikuniuliza kama niliyaelewa mashtaka, isipokuwa ilinieleza tu kuwa sitakiwi kujibu chochote, mara ikatoa tarehe nyingine ya kutajwa, Agosti 5, 2021,” akadai kiongozi huyo wa upinzani.