Mbowe na wenzake wasomewa mashtaka sita ikiwemo kukutwa na sare ya jeshi, bastola

Mbowe na wenzake wasomewa mashtaka sita ikiwemo kukutwa na sare ya jeshi, bastola

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamesomewa upya mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo vya kigaidi.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamesomewa upya mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo vya kigaidi.

Mashtaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria.

Mbowe na wenzake wasomewa mashtaka sita ikiwemo kukutwa na sare ya jeshi, bastola

Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili fedha kwa ajili vitendo vya kigaidi.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Ijumaa, Agosti 6, 2021 na jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akiwasomea mashtaka hayo, wakili Hilla amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2020.

Amedai katika kosa la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kula njama za kutenda kosa, tukio wanadaiwa kulitenda kati ya Mei Mosi, 2020 na Agosti Mosi 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la  Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, walitenda kosa hilo.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa walikula njama za kulipua vituo mbalimbali vya mafuta na katika mikutano isiyokuwa ya kisiasa na kusababisha hofu kwa wananchi kwa lengo la kuutishia umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Shtaka la pili ni kufadhili vitendo vya kigaidi, linalomkabili Mbowe ambapo anadaiwa katika tarehe hizo, katika hoteli  ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la  Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, Mbowe aliwafadhili Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya, huku akiwa na lengo la ufadhili huo utatumikia katika kutekeleza vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo ya mafuta na mikusanyiko ya wananchi.

Mbali na Mbowe, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, washtakiwa wengine ni Halfan Hassa, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

Washtakiwa baada ya kusomewa amshtaka hayo hawakutakiwa kujibu chochote na Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2021 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande, kutokana mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa walikuwa wanatetewa na jopo la mawakili, tisa wakiongozwa na Peter Kibatala.