Mkunga asimamishwa kazi kwa kutelekeza wajawazito

Muktasari:

Mkunga wa zahanati ya Kashai iliyopo Manispaa ya Bukoba, Leticia Muganyizi amesimamishwa kazi kwa kipindi cha miezi mitatu na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania kwa kosa la kutelekeza akina mama wajawazito.

Dar es Salaam. Mkunga wa zahanati ya Kashai iliyopo Manispaa ya Bukoba, Leticia Muganyizi amesimamishwa kazi kwa kipindi cha miezi mitatu na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania kwa kosa la kutelekeza akina mama wajawazito.

Tukio hilo lililotokea jana Julai Mosi, 2022 limesababisha adha kwa wajawazito hao na hivyo kukiuka sheria ya uuguzi na ukunga yam waka 2010 kifungu cha 25 (2)(a) na (3)(f)(k) pamoja na kanuni na misingi ya maadili ya kitaaluma ya wauguzi na wkaunga Tanzania kwamba ni marufuku kumtelekeza mgonjwa, mgonjwa anapaswa kupata huduma salama, zenye ubora na staha.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Juni 2 na Msajili wa Baraza hilo, Agnes Mtawa imeeleza kuwa mkunga huyo pamoja na mhudumu walikataa kuwafungulia mlango akina mama wajawazito wawili waliofika kujifungua usiku kwa madai ya kuhofia usalama wao.

“Baraza limesikitishwa na kulaani kitendo kilichofanywa na watumishi wa zahanati ya Kashai akiwemo muuguzi na mkunga pamoja na mhudumu, licha ya viongozi mbalimbali wa Serikali kufika kituoni hapo na kuwathibitishia watumishi hao usalama, bado walikaidi kufungua mlango kutoka nje na kutoa huduma kwa akina mama hao,” amesema Mtawa.

Mtawa amesema amesimamisha kazi mkunga huyo kwa kipindi cha miezi mitatu kwa mujibu wa kanuni ya 7 (1) ya kutoa huduma za uuguzi na ukunga muuguzi huyo wakati shauri hilo likishughulikiwa kisheria na kitaaluma.

Pia ametoa maagizo, “Mtumishi mwingine nashauri Mamlaka inayowasimamia wahudumu wa afya kumshughulikia.”