Mlinzi hoteli gari la Chadema ilikonusurika kuteketea mbaroni

Muonekano wa gari la Chadema lililonusurika kuteketea kwa moto wilayani Chato.

Muktasari:

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amemtaja mlinzi anayeshikiliwa kuwa ni Ciprian Dundaki (36) ambaye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuubaini moto huo Saa 8:00 usiku wa kuamkia Agosti 2, 2023.

Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mlinzi wa hoteli ya Twiga eneo la Buzrayombo Wilaya ya Chato kwa mahojiano kuhusu tukio la gari la matangazo la chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kunusurika kuteketea kwa moto.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amemtaja mlinzi anayeshikiliwa kuwa ni Ciprian Dundaki (36) ambaye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuubaini moto huo Saa 8:00 usiku wa kuamkia Agosti 2, 2023.

Amesema timu ya upelelezi ya jeshi hilo linaendelea kufanya mahojiano na watu mbalimbali kufahamu chanzo cha moto huo uliodhibitiwa mapema na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Chato waliofika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa uongozi wa hoteli.

“Hadi sasa hatufahamu chanzo cha moto. Tunasubiri taarifa ya kitaalam kutoka kwa wenzetu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Tunamshukuru Mungu hakuna madhara yoyote ya kibinadamu iliyotokana na tukio hilo,’’ amesema Kaimu Kamanda Maro

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wakati moto huo unagundulika, viongozi na maofisa wa Chadema hawakuwepo hotelini hapo kwa sababu walilala eneo lingine baada ya kukosa nafasi hoteli ya Twiga.

‘’Baada ya kukosa nafasi ya kulala kutokana na vyumba vyote kujaa, wale watu wa Chadema waliomba na kuruhusiwa kuhifadhi gari lao eneo la maegesho ya hoteli ya Twiga ambalo licha ya kuwa na ulinzi, pia lina uzio wa usalama,’’ amesema kiongozi huyo wa Polisi

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Chato, Maneno Ramadhan amesema baada ya kufanikiwa kuudhibiti moto huo, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto huo.

‘’Tunaendelea na uchunguzi kubaini chanzo ha moto,’’ amesema Kamanda Ramadhan

Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakharia Obad amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufika mapema na kuudhibiti moto huo huku akiviomba vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo na wahusika kutokana na hisia kwamba tukio hilo lina viashiria vya kisiasa.

Amesema Chadema inahusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa kwa sababu muda mfupi kabla ya gari lao kunusurika kuteketea kwa moto, watu wasiojulikana walivamia na kuharibu jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya mkutano wa hadhara katika eneo la Mganza uliotarajiwa kuhutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu.