Mloganzila kuongeza shepu, matiti

Muktasari:
- Hatimaye wanawake waliokuwa na matamanio ya kupunguza au kuongeza maumbile yao ikiwemo ukubwa wa matiti na makalio, kupunguza tumbo au nyama kwenye mikono na sehemu nyingine za mwili, wamefikiwa baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kuanza huduma hiyo mapema mwezi huu.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inatarajia kufanya huduma za kibingwa bobezi za upasuaji wa kupunguza uzito na upasuaji rekebishi (Bariatric and Reconstructive Surgery) kuanzia Oktoba 27 mwaka huu.
Upasuaji huo utahusisha kupunguza mafuta ya mwilini na kurekebisha maungo ikiwemo kupunguza au kuongeza ukubwa wa matiti na makalio, kupunguza tumbo au nyama kwenye mikono na sehemu nyingine za mwili.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 10, 2023 na Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Dk Eric Muhumba alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu upasuaji huo.
Dk Muhumba amesema upasuaji huo utafanywa na wataalamu wa Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa upasuaji wa kupunguza uzito na upasuaji rekebishi kutoka India, Dk Mohit Bhandari pamoja na Taasisi ya Afya ya MedINCREDI .
Amesema huduma hizo za kupunguza uzito zinafanyika kwa kupunguza nafasi ya kuhifadhi chakula kwa kushona sehemu ya eneo la tumbo kitu kitakachosababisha mtu kutumia kiasi kidogo cha chakula hivyo kupunguza uzito.
Dk Muhumba ameeleza kuwa katika kutoa huduma hizo, watatumia njia ya kisasa ambayo haitahusisha upasuaji ambapo watatumia kifaa maalumu kiitwacho endoskopia kuingia katika tumbo na kupunguza nafasi ya tumbo la chakula.
“Upasuaji huu utafanyika kwa bei nafuu sana ukilinganisha na endapo mtu angeenda kutafuta huduma hizi nje ya nchi, hivyo tumeamua kuwasogezea wananchi huduma hizi na kuwapunguzia usumbufu wa wananchi kusafiri nje ya nchi kutafuta huduma hizi,” amesema Dk Muhumba.
Sambamba na huduma hizo Dk Muhumba ameongeza kuwa huduma rekebishi itahusisha kurekebisha kwa kupunguza mafuta na kurekebisha sehemu ya mwili mfano kupunguza au kuongeza ukubwa wa matiti, nyama kwenye mikono na sehemu nyingine mbalimbali za mwili.