Mmarekani aliyejipatia kitambulisho cha Nida ahukumiwa

Muktasari:

  • Mbali na adhabu hiyo, Mahakama hiyo imeamuru mshtakiwa huyo kurudishwa nchini kwako.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu raia wa Marekani, Yaki Lee (45), kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita, baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka manne likiwemo la kutoa taarifa za uongo na kujipatia kitambulisho cha Taifa (Nida).

Lee maarufu kama Yaki Khalid Juma, amehukumiwa kifungo hicho, leo Septemba 25, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi, baada ya kukiri mashtaka yake.

Mbali na adhabu hiyo, Mahakama hiyo imeamuru mshtakiwa huyo kurudishwa nchini kwao.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini na hivyo kukwepa kifungo.

Mshtakiwa huyo ametiwa hatiani baada ya wakili wa Serikali, Shija Sitta kumkumbusha mashtaka yake na kisha kukiri mashtaka yake na kuomba apunguziwe adhabu.

"Mshtakiwa umetiwa hatiani kama ulivyoshtakiwa baada ya kukiri mashtaka yako manne, hivyo mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita kwa kila kosa," amesema Hakimu Kyaruzi.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa hukumu hiyo mshtakiwa aliiomba mahakama imupunguzie adhabu na hatarudia kosa hilo.

"Mheshimiwa hakimu najutia kwa sababu nilikuwa sijui naomba mahakama yako inisamehe sana, hivyo naomba unipunguzie adhabu," amedai Juma.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili Shija aliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo na wala asipewe kifungo mbadala.

Katika kesi ya msingi, Juma anakabiliwa na kesi ya jinai namba 169/2023.

Katika shtaka la kwanza, mashtaka  anadaiwa Septemba14, 2023 katika Ofisi za Uhamiaji za Ilala jijini hapa,  mshtakiwa alibainika kuishi nchini bila kuwa na nyaraka zinazoonyesha uhalali wake.

Shtaka la pili, siku, tarehe na eneo hilo, mshtakiwa huyo akiwa raia wa Marekani anadaiwa alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa uhamiaji kuhusu utaifa wake kwa lengo la kujipatia hati ya kusafiria ya Tanzania.

Pia, siku, tarehe na eneo hilo, mshtakiwa aliwasilisha nyaraka za kugushi kwa lengo la kujipatia cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha Taifa cha Tanzania (Nida).

Shtaka la nne, mshtakiwa kupitia nyaraka hizo za uongo, anadaiwa kujipatia kitambulisho cha Nida, kinyume cha sheria.