Mnaijeria kortin akituhumiwa kusafirisha kilo 4 za Heroine

Muktasari:
- Raia wa Nigeria, Eze Amos (38), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina Heroin, zenye uzito wa kilo 4.14.
Dar es Salaam. Raia wa Nigeria, Eze Amos (38), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina Heroine, zenye uzito wa kilo 4.14.
Amos, ambaye ni Mkazi wa Gongolamboto, amefikishwa Mahakamani hapo leo Oktoba 6, 2023 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 46/2023.
Mshtakiwa huyo alisomewa shtaka lake na wakili wa Serikali, Eric Davis, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.
Awali, kabla ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Ruboroga alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Akimsomea hati ya mashtaka, Wakili Davis, alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa lake, Agosti 31, 2019 eneo Ubungo, Wilaya ya Ubungo
Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa anadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 4.14, kinyume cha sheria.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wapo katika hatua za kuwasilisha taarifa muhimu Mahakama Kuu, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Ruboroga baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 20, 2023 itakapotajwa.
Mshtakiwa alirudishwa rumande kwa sababu shtaka linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.