Mpango aagiza TLS kudhibiti mawakili vishoka

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philip Mpango
Muktasari:
- Mkutano huo wa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaofanyika kwa siku tatu huku ukilenga pia kufanya uchaguzi wa viongozi wa juu wa chama hicho.
Arusha. Makamu wa Rais Philip Mpango ameonyesha kukerwa na vishoka wanaojifanya mawakili na kuwatapeli wananchi wanaotafuta haki zao kupitia msaada wa kisheria.
Kufuatia hilo, Mpango ameziagiza taasisi zote za serikali na binafsi kuhakikisha zinatumia mihuri ya kielectoriki katika kazi za uwakili ili kuwaondosha vishoka wa uwakili.
Mpango ameyasema hayo leo May 11, 2023 wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaoendelea mkoani Arusha.
"Mimi naamini kama mkiheshimu na kulinda taaluma yenu mtaondokana na tabia hii ya vishoka, sasa hakikisheni mnashirikiana na wizara ya sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu swala hili la uwepo wa mihuri ya kieletroniki ili kudhibiti matapeli wanaotumia mihuri isiyo halali kufanya kazi za uwakili" alisema
Mpango pia aliwataka mawakili kufanya kazi zao kwa kuzingatia na kuheshimu maadili ya taaluma ya Sheria kwa kuepuka kupokea rushwa kutoka upande wa pili na hivyo kuwasaliti wateja wao ambao kimsing waliwaamini na kuwapa kazi.
"Sheria ni moja ya taaluma yenye heshima kubwa hapa duniani, hivyo inahitaji kiwango kikubwa cha uadilifu na maadili mema, lakini kumekuwa na tuhuma za baadhi yenu kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwa maslahi yenu binafsi, na hivyo kuwasaliti wateja wenu na kuharibu kesi, naomba muache"
Mpango alitumia nafasi hiyo kuwataka TLS na kamati ya mawakili kuchukua hatua kali za kinidhamu na za kisheria dhidi ya mawakili wachache wanaoharibu heshima ya taaluma hiyo kwa kukosa uadilifu na maadili mema.
"Mategemeo ya wananchi wengi ni kuwa mlichagua kuwa mawakili kwa sababu mnapenda haki na kutetea wanyonge sio kwa sababu ya kupenda pesa hivyo TLS wachukulieni hatua watakaobainika ili kuwakumbusha majukumu yao vema," ameshauri Mpango.
Kwa upande wake Rais wa TLS Prof Edward Hoseah, ameiomba serikali kuwapatia fedha za kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao binafsi ikiwemo msaada wa kisheria kwa wananchi wanaokosa haki kutokana na changamoto hiyo.
Zaidi ameiomba Serikali kuwalipa ada mawakili wake sambamba na kuwapatia eneo la uwekezaji katika mkoani Arusha, itakaiwezesha TLS kupatia kipato ili kitumike katika kuwasaidia wananchi kupata haki zao kwa huduma bure za kisheria sambamba na kampeni ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
"Kwa mwaka tunaweza kuwasaidia wananchi 7307 msaada wa kisheria na huduma za uwakili wasio na uwezo wa kugharamia hivyo tunaomba Serikali itupe sapoti zaidi ili kujenga jamii yenye amani na utulivu kwa sababu ya upatikanaji wa haki zao"
Nae waziri mwenye dhamana ya Sheria, Damas Ndumbaro aliwataka mawakili hao kutumia ujuzi, maarifa na taaluma yao katika kusaidia utekelezaji wa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya itakayosaidia taifa kwa miaka 100.