Mpango wa maendeleo wa miaka mitano kugharimu Sh114 trilioni

Mpango wa maendeleo wa miaka mitano kugharimu Sh114 trilioni

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/22 hadi 2025/26) unakadiriwa kugharimu Sh114.8 trilioni.


Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/22 hadi 2025/26) unakadiriwa kugharimu Sh114.8 trilioni.

Utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/17 hadi 2020/21) ulikadiriwa kutumika Sh107 trilioni.

Akiwasilisha mpango huo bungeni leo Alhamisi Aprili 8,  2021, Dk Mwigulu amesema fedha hizo zinajumuisha mchango wa sekta binafsi wa Sh40.6 trilioni na sekta ya umma Sh74.2 trilioni kutoka vyanzo vya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, misaada na mikopo.

Pia, amesema  vyanzo mbalimbali bunifu vinavyoweza kutumika kugharamia shughuli za maendeleo vimeanishwa vikiwamo vya ugharamiaji wa pamoja, hati fungani za mashirika, mitaji binafsi na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Pia, amesema baraza la Taifa la biashara litaratibu na kusimamia ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango na washirika wa maendeleo watahamasishwa kushiriki katika utekelezaji wa mpango kupitia vikao rasmi vya ushirikiano.