Mpina amvaa Tizeba bungeni

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na Naibu wake Abdallah Ulega baada ya bunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma leo.Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amemvaa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk Charles Tizeba kuwa anawanyanyasa watumishi wa wizara hiyo pamoja na uamuzi wa kusamehe kodi kwa miezi sita na kusababisha hasara ya Sh5 bilioni.

Dodoma.Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amemvaa Dk Charles Tizeba kuwa kitendo chake kutoa msamaha (holiday) ya miezi sita kwa wawekezaji kutoa mrabaha Dola za Marekani 0.4 kwa kila kilo ya samaki, kumeingiza hasara ya Sh5 bilioni.

Mpina ameyasema hayo leo Jumatano  Mei 22 2019 bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020. 

Wabunge waliozungumzia kuhusu mrabaha  huo kukwamisha mapato yanayotokana na bahari kuu ni pamoja na Saada Mkuya (Welezo-CCM).

Amesema Serikali ya awamu ya nne hakuna namna inavyoweza kumuonea mtu na kwamba, sheria zote ambazo Serikali inatekeleza, zimetungwa na Bunge.

Amesema wakati mwingine hata wabunge hugeukana anapokamatwa mtu aliyekuwa na uhusiano naye wa karibu.

“Amezungumza hapa mheshimiwa Tizeba, Tizeba alikuwa waziri wa mifugo na uvuvi. Lakini hata hili la kuzungumza kuwa vijana wanawaonea watu wake sio kweli.

“Mheshimiwa Tizeba amekuwa akipigia simu vijana wa mifugo na uvuvi kuwaharasi na kuwaambia akiwa waziri hataki watu wake wakamatwe kwa uvuvi haramu.”

Amesema amekuwa akiwanyanyasa pia watumishi wa wizara hiyo hata sasa akiwa mbunge akisema hataki mtu wake akamatwe.

“Sasa ukifika hapa unabadilika kwa sababu hawa vijana hawako ndani ya Bunge hili unawashutumu kwa kiwango hicho, siyo vizuri. Vijana wetu wanafanya kazi vizuri , lakini kama wakifanya vibaya tuletee tutawashughulikia tu,” amesema.

Akizungumzia kuhusu mrabaha wa Dola za Marekani 0.4, Mpina amewataka wabunge kuitendea haki nchi kwa sababu hilo jambo limeanzia ndani ya Bunge.

“Watu walikuja na meli zenye ukubwa wa hadi tani 300, wanalipa leseni ya Dola za Marekani 65,000 peke yake. Mbona hamjajiuliza akivuliwa hapa anauzwa shilingi ngapi hadi waseme kuwa tuiondoe hiyo 0.4,” amehoji.

Amesema Bunge ndiyo waliliambia Serikali kuwa wamechoka kudhulumiwa na kuonewa na meli za uvuvi zinazotoka nje ya nchi.

Amesema baada ya kuingia Serikali ya Awamu ya Tano ilitekeleza kwa kubadili kanuni mwaka 2016 kwa kuweka mrahaba wa dola za marekani 0.4.

“Waziri aliyekuwepo mheshimiwa Tizeba alitoa holiday ya miezi sita wasilipe 0.4, alipotoa likizo ya O.4 kamati ya Bunge ikabaini dosari na Tanzania imepoteza  Sh5 bilioni kwa holiday ile.

“Leo mnageukaje O.4 ni makosa na Serikali ilifanya njama ya kuhujumu uvuvi bahari kuu.  Itendeeni haki Serikali yenu. Hii Serikali ni ya kwenu, hii mheshimiwa waziri mwenzangu ndiye aliyeiweka,” amesema.

Hata hivyo, kauli ya kuwa Dk Tizeba anamlaumu hakuitoa tozo , ilizua minong’ono bungeni na Spika Job Ndugai aliwataka wabunge kusikiliza kwa sababu mtu anayetajwa yupo bungeni, hivyo anaweza kujitetea.

“Waziri aliyekuwepo aliweka kanuni na jana aligeuka kuwa mlalamikaji ya kwamba mimi nime- frastuate (nimevuruga) kwa 0.4. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni , itendeeni haki Serikali, mmeiweka wenyewe kwa nia njema ili Taifa liweze kunufaika,” amesema.

Amesema ni lazima kutafakari kwanza kabla ya kuondoa mrabaha huo kwa kuangalia mbadala wa hilo na Taifa litanufaikaje.

Hata hivyo, amesema wakati wanaanza operesheni ya uvuvi haramu, walikamata meli 24 kwa kujihusisha na uvuvi haramu.