Mpina ataka ujenzi SGR uchunguzwe

Muktasari:

  • Wakati ujenzi wa Reli ya Kisasa ukiendelea katika maeneo mbalimbali, Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina ametaka kufanyika kwa uchunguzi wa mchakato wa zabuni wa kipande cha Tabora hadi Kigoma baada ya kuwa na mzabuni mmoja.

Dodoma. Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina ametaka kuundwa kwa timu ya uchunguzi ili kuchunguza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika kipande cha Tabora hadi Kigoma baada ya kubaini gharama za ujenzi ni kubwa kuliko vipande vingine kwa Sh3.4 bilioni kwa kilometa.

Mpina ameyasema hayo leo Jumanne Januari 31, 2023 wakati akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.

Amesema mkataba uliingiwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ya nchini China kwa utaratibu wa mshindani wa zabuni mmoja ambapo gharama zilikuwa ni Sh6.34 trilioni.

“Unahurusuje mfumo wa mzabuni mmoja ambao hauruhusu ushindani. Anaweza kuliamua analolitaka…aliingia mkataba wa Tabora hadi Kigoma lakini wakati huo huo alishapewa mkataba wa Mwanza kwenda Isaka wa Kilometa 341 kwa Sh3.12 trilioni,” amesema.

Amehoji unawezaje kuipa mkataba mwingine wa ujenzi wa Kilometa 506 wakati inamkataba mwingine na haijawahi kujenga hata kilometa moja.

Amesema kipande cha Kigoma hadi Tabora ndio kina gharama kubwa kuliko vipande vingine ambapo wastani wa gharama za ni kilometa moja Sh9.1 bilioni kwa upande wa Mwanza kwenda Isaka lakini kwa upande wa Tabora hadi Kigoma ni Sh12.5 bilioni kwa kilometa moja.

Amesema hilo limeweka uwepo wa tofauti ya Sh3.4bilioni kwa kilometa na mbaya zaidi wakati watalaam wanafanya usanifu wa kina katika kipande cha Tabora hadi kigoma walipaini kingeweza 4.89 trilioni na Sh6.4 trilioni ikiwa ni tofauti ya Sh1.5 trilioni.

“Hivi karibuni Serikali imesaini mkataba huo licha Bunge kutoa tahadhari. Mimi napendekeza kuwasilisha taarifa mchakato wa manunuzi bungeni kuanzia utangazaji wa zabuni na tathimini ya utoaji wa zabuni,” amesema.

Amesema taarifa hiyo iwasilishwe kwa kamati za Bunge zaMiundombinu na Katiba na Sheria na pia Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi (PPRA) waunde timu ya pamoja.

Amesema timu hiyo iende kukagua mradi huo wa Tabora hadi Kigoma na kisha kutoa taarifa za ukaguzi wa kile kilichofanyika.