Mpina bungeni hadi Novemba

Muktasari:

  • Adhabu imeamuliwa na wabunge wengi kupitia kura baada ya Mpina kushindwa kuthibitisha madai yake dhidi ya Waziri wa Kilimo.

Dodoma. Bunge limemsimamisha mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kuhudhuria vikao 15 hadi Bunge la Novemba, 2024.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Mpina hatahuduria vikao vitano vya Bunge hili la Bajeti kuanzia leo, pia hatahudhuria Bunge lijalo la Septemba ambalo lina vikao tisa.

Amesema vikao vitano vya Bunge la Bajeti na vikao tisa vya Bunge la Septemba inakuwa ni vikao 14 na kwamba, Mpina hatahudhuria kikao kimoja cha Bunge la Novemba 2024 na adhabu itaishia hapo na ataanza kuhudhuria kikao cha pili cha Bunge hilo la Novemba.

Pia, Spika amesema Mpina hataruhusiwa kufika kwenye maeneo ya Bunge wala kujihusisha na shughuli zozote za Bunge.

Azimio la Bunge limefikiwa leo Jumatatu Juni 24, 2024 baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Ally Makoa kulieleza Bunge kwamba, Mpina amekutwa na hatia ya kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge.

Uamuzi wa kumfungia Mpina kuhudhuria vikao 15 umefikiwa na wabunge wengi kwa kupiga kura ya kuitikia ndio.

Dk Tulia baada ya wabunge kuchangia aliwauliza wanataka Mpina afungiwe kwa vikao 10 kama lilivyo pendekezo la Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, waliitikia wachache.

Alipouliza wabunge wanaotaka Mpina afungiwe kwa vikao 15 waliitikia wengi huku pendekezo la kufungiwa kwa vikao 20 halikupendekezwa na mbunge yeyote.

Spika baada ya kutangaza uamuzi huo alimtaka Mpina kukusanya vitu vyake na kutoka kwenye ukumbi wa Bunge.

Uamuzi wa kumfungia Mpina umefikiwa baada ya Spika Tulia kwanza kumwagiza apeleke ushahidi bungeni baada ya kumtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwamba amesema uongo bungeni na amevunja sheria.

Spika alitoa uamuzi huo Juni 4, 2024 kwamba ushahidi huo wa Bashe kusema uongo uwe umefika kwake Juni 14, 2024.

Hata hivyo, Mpina baada ya kuwasilisha ushahidi huo siku hiyo hiyo alizungumza na waandishi wa habari kuelezea ushahidi wake alioupeleka kwa Spika.

Baada ya Mpina kuwasilisha ushahidi wake kwa Spika uliotolewa na baadhi ya vyombo vya habari, Juni 18, 2024 Spika alimpeleka kwenye Kamati ya Maadili kwa kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge, kwa kupeleka ushahidi nje ambao ulikuwa bado haujafanyiwa kazi na Spika na Bunge.

Spika aliiagiza Kamati ya Maadili kushughulikia hilo na kutoa taarifa leo Juni 24, 2024 mbele ya Bunge.

Wabunge wengi waliochangia walitaka Mpina apewe adhabu kali huku wengine wakisema suala hilo watalipeleka kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) inayotarajia kukutana Juni 30, 2024.

Wabunge waliosema watampeleka NEC ya CCM ni wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku 'Musukuma' na mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji.

Pia, Musukuma amesema Mpina siyo mara ya kwanza kudharau Bunge kwa kuwa alipokuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alipeleka maofisa wa wizara kwenye kantini ya Bunge kupima urefu wa samaki kwa rula.

Hata hivyo, baadaye Mpina aliomba radhi Bunge na Spika wa wakati huo, Job Ndugai alimsamehe.

Mbunge wa Kasulu Vijijini, Vuma Augustine mbali na kumtaka Mpina aliombe radhi Bunge, pia aliwaomba wabunge wenzake wamshauri ajiuzulu ubunge ili apate nafasi ya kulisema Bunge na Spika akiwa nje.

Wabunge wengine waliochangia ni Hamis Tabasamu (Sengerema) na Godwin Kunambi (Mlimba) ambao pia walimtaka Mpina aombe radhi Bunge.

Wengine ni Katani Katani (Tndahimba),  Mariam Ditopile (Viti Maalumu), Elibariki Kingu (Singida Magharibi), Tauhida Gallos na Cecilia Pareso (Viti Maalum). Wengine ni Profesa Patrick Ndakidemi (Moshi Vijijini) na Josephat Gwajima (Kawe).