Mradi Sh27 bilioni kumaliza shida ya Maji vijiji 17 Monduli

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza katika hafla ya kusainiwa Miradi miwili ya Maji Monduli.

Muktasari:

  • Huenda changamoto ya upatikanaji wa maji katika vijiji 17 wilayani Monduli ikabaki historia.

Monduli. Changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji 17 wilayani Monduli mkoani Arusha, itabaki historia iwapo Serikali itakamilisha mradi utakaogharimu Sh27 bilioni, uliyosainiwa leo.

Kusainiwa kwa mradi huo, kunatajwa kuwa tumaini jipya kwa wakazi wa vijini hivyo ambao mara zote hutumia maji ya mabwawa kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Akizubgunza katika hafla ya kusainiwa kwa mradi huo katika Kata ya Lepurko wilayani humo leo, Novemba 12, 2023 Waziri wa Maji, Juma Aweso amesema hatua hiyo imetokana na Serikali kusikia kilio cha wananchi.

Katika maelezo yake, Aweso amewataka wakandarasi watakaotekeleza mradi huo kuhakikisha wanaifanya kazi hiyo kwa haraka na wakati.

Kuhusu kilichosaiwa, amesema ni mikataba miwili ambayo ni mradi wa maji toka jiji la Arusha kwenda vijiji 13 utakaogharimu Sh20 bilioni na mradi wa maji wa vijiji vinne vya Makuyuni utaogharimu Sh7 bilioni.

Meneja wa Mamlaka ya Maji vijijini (RUWASA) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Joseph Makaidi amesema mradi huo utatekelezwa kwa miaka miwili huku wananchi nao wakielezea matumaini yao kutokana na mradi huo.

"Ndani ya miaka miwili mradi huu utakuwa umekamilika lakini ndani ya kipindi hicho tunaamini Maji yataanza kupatikana," amesema.

Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa amesema wanamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo wa kihistoria Monduli.

Lowassa amesema shida ya Maji ni kubwa Wilaya ya Monduli na hivyo mradi huo utaondoa adha hiyo.

Mmoja wa wananchi wa Lepurk, Jane Lowassa amesema, "Hapa tuna shida kubwa ya MajiĀ  tumekuwa tukitumia Maji ya Mabwawa sisi na Mifugo pamoja," amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isack Joseph ametaka Serikali isiishie vijiji hivyo tu, ichukue hatua kama hiyo katika maeneo mengine yenye changamoto.