Mradi wa maji wa Sh465 milioni Handeni wakamilika
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, akimtwisha ndoo kichwani mmoja wa wananchi wa Kata ya Kideleko, Wilaya ya Handeni, wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa maji uliokamilika, uliofanyika wilayani humo. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- Zaidi ya wananchi 6,000 wa Kata ya Kideleko, Handeni Mji, wameondokana na adha ya kutembea kilomita 10 kutafuta maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji
Tanga. Adha ya kutembea hadi kilomita 10 kutafuta maji kwa wakazi wa Kata ya Kideleko, Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga imeanza kuwa historia.
Hiyo ni baada ya kukamilika na kukabidhiwa mradi wa maji wenye thamani ya Sh465.2 milioni utakaowanufaisha wananchi 6,037.
Mradi huo unahudumia maeneo ya Kideleko, Kampene, Muungano, Ndekai na Bangu; na umetekelezwa na WaterAid Tanzania kwa ufadhili wa OKF kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM) pamoja na Halmashauri ya Mji Handeni.
Mradi huo umekabidhiwa leo Ijumaa, Julai 3, 2026, kwa Serikali.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi, usafi wa mazingira na usafi binafsi.
"Ushirikiano huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na salama, jambo ambalo ni msingi wa maendeleo ya afya, elimu na uchumi wa jamii," amesema.
Amewataka Ruwasa, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni, viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya mradi huo ili huduma iendelee kutolewa kwa ufanisi kwa muda mrefu.
Mradi huo umegharimu Sh465,182,915.20 na umehusisha ujenzi wa chujio la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000, tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji lenye urefu wa mita 1,485 pamoja na mabomba ya usambazaji yenye urefu wa mita 2,358.
Pia, umejumuisha ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji vinavyotumia mfumo wa malipo ya kabla (prepaid), hatua inayolenga kuboresha uendelevu wa huduma hiyo.
Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga amesema mafanikio ya mradi huo yatategemea usimamizi mzuri wa miundombinu ili uwekezaji uliofanywa uendelee kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
"Usimamizi mzuri wa miundombinu hii utalinda uwekezaji uliofanywa na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaendelea kupata huduma ya maji kwa ufanisi," amesema.
Kwa wakazi wa Kideleko, mradi huo unatarajiwa kubadilisha maisha yao baada ya miaka ya kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Mkazi wa eneo hilo, Juma Abdallah amesema kabla ya kukamilika kwa mradi huo wananchi walilazimika kutembea hadi kilomita 10 kutafuta maji, hali iliyowaathiri watoto katika masomo na kupunguza muda wa familia kufanya shughuli za uzalishaji mali.
"Tulikuwa tunatembea kilomita 10 kila siku kutafuta maji. Watoto walichelewa shule, wengine walikosa kabisa masomo, na sisi tulipoteza muda wa kufanya shughuli za kutafuta kipato. Sasa tunaamini maisha yetu yatabadilika," amesema.
Naye Lydia John amesema wanawake na watoto ndio waliobeba mzigo mkubwa wa kutafuta maji kila siku, jambo lililowaongezea uchovu na kupunguza muda wa kushiriki shughuli nyingine za maendeleo.
Amesema huduma ya maji kusogezwa karibu na makazi itaongeza muda wa watoto kujifunza, kuboresha shughuli za kiuchumi za familia na kuinua ustawi wa jamii.
"Kutembea kilomita 10 kila siku ilikuwa changamoto kubwa kwa familia zetu. Sasa watoto watapata muda wa kusoma na sisi tutatumia muda wetu kufanya shughuli za maendeleo badala ya kutafuta maji siku nzima," amesema.