Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mrithi wa Ekelege ‘amkaanga’ kortini

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Viwango nchini, Charles Ekelege (katikati) akitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, baada ya kuahirishwa kwa kesi yake ya matumizi mabaya ya ofisi, jana. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Kuhusu taratibu za fedha, shahidi huyo alidai zilikuwa zinaongozwa na kanuni za fedha za 2005 ambazo zilitumika hadi 2010 na kwamba, zilikuwa na ukomo katika fedha, matumizi ya maendeleo, uzalishaji mali ya umma na kusamehe madeni.

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Joseph Masikitiko ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa msamaha uliotolewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Charles Ekelege ulikiuka kanuni za fedha.

Masikitiko aliyaeleza hayo jana wakati akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machulya kutoa ushahidi wake dhidi ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka.

Anadaiwa kuondolea ada ya asilimia 50 Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali na Quality Motors, bila kupata kibali cha bodi.

Akitoa ushahidi wake, alidai kitendo cha mkurugenzi huyo wa zamani wa TBS kutoa msamaha bila kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi wa shirika ni kukiuka kanuni za fedha.

Alidai kuwa licha ya kukiuka kanuni za fedha, wakati wa kikao cha bodi ya wakurugenzi Juni 30, 2011, Ekelege alikiri kosa hilo na kwamba Mwenyekiti wa Bodi alimsamehe na kuonya kosa kama hilo lisirudiwe tena.

“Mwaka 2007/09, nilikuwa Meneja wa Fedha na Utawala, majukumu yangu yalikuwa kusimamia masuala ya fedha, utawala, rasilimali watu, ununuzi na matengenezo.” alieleza.

Alidai mfumo wa utendaji wa shirika hilo ulikuwa ukiongozwa na mkurugenzi, mameneja wawili na wakuu wa idara wanne ambao kwa pamoja waliunda timu ya utawala.

Kuhusu taratibu za fedha, shahidi huyo alidai zilikuwa zinaongozwa na kanuni za fedha za 2005 ambazo zilitumika hadi 2010 na kwamba, zilikuwa na ukomo katika fedha, matumizi ya maendeleo, uzalishaji mali ya umma na kusamehe madeni.

Aliendelea kuwa ili kuweza kusamehe, lazima uangaliwe uwezo wa mhusika, jitihada alizotumia kuomba msamaha na kwamba, lazima maombi hayo yapelekwe kwa mkurugenzi ambaye atapelekwa kwa Mhasibu Mkuu naye atampelekea Mkaguzi wa Ndani ambaye atapitia na kutoa mapendekezo au vigezo vinavyokidhi kusamehe.

Alidai kuwa hakuwahi kufahamu kama mkurugenzi wake, Ekelege aliondolea ada ya asilimia 50 kampuni hizo hadi alipoiona ripoti ya mkaguzi wa ndani ya mwaka 2008/09.

Awali akisomewa maelezo ya awali, Ekelege alikubali kuwa aliwahi kuwa mwajiliwa wa TBS kama Mkurugenzi Mkuu kati ya Novemba 2007 na mwaka 2012, aliwahi kuwa kati ya wajibikaji kwenye majumuisho ya huo mkataba katika masuala ya kifedha na biashara.

Pia alikubali kutoa leseni kwa kamapuni za Jaffar Mohamed Ali Garage ya Dubai, Quality Motors ya Lot 3 Wang Toi Shan, Hung Mo Tam Pat Heung, Hong Kong zitumike kama Nembo ya Shirika la Viwango TBS ili iweze kukagua magari na kuyakataa yote yaliyobakia.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unatarajia kuwaita mashahidi saba kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo pamoja na kuwasilisha vielelezo 10 ambavyo vinaweza kutumika kama sehemu ya ushahidi iwapo havitakuwa na kipingamizi.

Katika kesi hiyo, Ekelege anadaiwa kuwa Machi 28, 2008 akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS kwa nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kuziondolea kampuni hizo ada yenye thamani ya Dola 42,543 za Marekani (Sh68,068,800).

Machulya alidai mshtakiwa aliziondolea ada kampuni hizo bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS.

Katika shtaka la pili, anadaiwa kutokana na kitendo hicho mshtakiwa alisababisha hasara ya Dola 42,543 za Marekani.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na yupo baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwasilisha fedha taslimu Sh35 milioni mahakamani hapo na kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika.