Mrundikano mama wajawazito wapatiwa suluhisho Chunya

Upande wa kushoto ni aliyevalia koti ya darkbkue ni Kaimu meneja wa Nyanda za Juu Kusini  Frank Rutakwa akimkabidhi vitanda Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka katika eneo la Hospitali ya Wilaya ya Chunya. Picha na Mary Mwaisenye

Muktasari:

  • Kina mama wajawazito Wilaya ya Chunya wapatiwa vitanda 12 na Benki ya NMB kupunguza changamoto ya mrundikano.

Chunya. Ili kupunguza changamoto ya mlundikano wa kina mama wajawazito wanaofika kupata huduma Hospitali ya Wilaya ya Chunya ambao kuna wakati  hulazimika kulala wawili kitandani  kimoja Benki ya NMB imetoa vitanda 12, viwili vya kujifungulia  na 10 vya kulala wagonjwa pamoja na viti mwendo saba kwaajili ya watoto wenye ulemavu vyote vikiwa na thamani ya Sh.9 milioni.

Akipokea vitanda hivyo pamoja viti mwendo Mkuu wa Wilaya Mayeka Mayeka ameishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan  kwa namna anavyoendelea kuboresha huduma za afya  kwa wananchi na kudai kuwa michango yao wanayoitoa inasaidia wananchi kupata huduma zinazostahili.

Mayeka amesema vifaa hivyo ilivyotolewa na Benki ni Sera  ya kurudisha faida kwa wananchi ambao ndio wateja wao hivyo vitawasaidia  kupunguza changamoto kwenye sekta ya Afya ya hususani hapo katika hospitali ya wilaya ambapo kuna wakati wakinamama wajawazito hulazimika kulala wawili kitanda kimoja na hii ni kutokana mji wa Chunya kuendelea kukua kwa kasi na kufanya mahitaji kuongezeka.

"Nawashukuru sana Benki ya NMB kwa huduma na mchango ambao mnatoa kwaajili ya kusaidia jamii katika sekta ya afya na elimu pia kwa kwendelea kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa Rais Samia Suluhu Hassan  kwani mchango huo utasaidia kupunguza changamoto.

Vituo vya afya vitakavyonufaika ni   Makongolosi Kituo cha Afya Kalangali pamoja na wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya Msingi Lupa,” amesema Mayeka.

Kaimu Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini wa National Bank of Commarce (NMB),  Frank Rutakwa  amesema kuwa suala la afya ni moja ya vipaumbele vyao kama Benki ili kuhakikisha afya za Watanzania wanaowahudumia zinakuwa bora,  hivyo faida wanayoipata kutoka kwa wateja wanarudisha kwenye jamii.

“Sisi kama Benki ya NMB afya ni kipaumbele chetu na ndiyo mana katika sekta ambazo tumejikita kusaidia Serikali ni pamoja na sekta ya afya. Pia tunaungana na Serikali yetu katika kuboresha sekta ya afya kama ambavyo  Rais wetu anaipa kipaumbele katika kuhakikisha kila kijiji na kila kata kunakuwa na kituo cha afya,’’amesema Rutakwa.

Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamimu Kambona ameishukuru NMB  kwa mchango  walioutoa ikiwa ni sehemu ya kile ambacho wanakipata  na kuahidi  kwamba wao kama halmashauri wataendelea kutoa ushirikiano kwa benki hiyo kama ambavyo wamekuwa wakishirikiana maeneo mbalimbali katika kulijenga Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Idara ya Afya Wilaya ya Chunya, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema  ameishukuru NMB  kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya afya  kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo wamevitoa  ili kuhakikisha wanaendelea kuwahudumia wananchi ipasavyo kwani afya ndio msingi wa uzalishaji mali si kwa mwananchi wa Chunya tu bali kwa  jamii  ya watanzania wote.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni  pamoja na  vitanda 10 vya kulazia wagonjwa, vitanda  2 vya kujifungulia kina mama wajawazito pamoja na viti mwendo saba kwaajili ya  wanafunzi wenye ulemavu ambapo vimepatikana ikiwa ni kutimiza lengo la benki hiyo ya kurudisha fadhira kwa wateja wake ambapo kila mwaka shughuli mbalimbali za kijamii wamekuwa wakizifanya.