Msafara wa Makonda wapata ajali Masasi, magari 10 yahusika
Muktasari:
- Msafara wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda uliokuwa ukitokea Songea umepata ajali maeneo ya Sululu wilayani Masasi mkoani Mtwara.
Masasi. Msafara wa magari wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda uliokuwa ukitokea mkoani Ruvuma kuelekea Dar es Salaam umepata ajali Kata ya Sululu wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara.
Katika ajali hiyo iliyotokea leo Jumapili, Februari 11, 2024 saa 8 mchana imehusisha magari zaidi ya 10 yaliyogongana sehemu ya nyuma katika eneo ambalo kuna kipande cha barabara ya vumbi.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Hamad Mtonga amesema baada ya msafara kufika eneo hilo, gari la mbele lilipunguza mwendo kutokana na vumbi ndipo magari ya nyuma yake yakaanza kugonganga kutokana na kuwa katika mwendokasi.
“Gari la mbele lilipunguza mwendo, lakini yale yaliyofuata yalikuwa na mwendo mkali, hawakujua kama mwenzao amepunguza mwendo, ndipo yaakaanza kugongana kila anayekuja anamgonga mwenzake,” amesema Mtonga ambaye ni kada wa CCM.
Kwa mujibu wa Mtonga, mwenyekiti wa Jumuiya wa Wanawake wa CCM (UWT) wilayani Tandahimba, Arafa Nakatanda na katibu mwenezi wa chama hicho wilayani humo, Jafari Hassan wamejeruhiwa na wamepelekwa hospitali.
Kwa mujibu wa mashuhuda, baadhi ya magari likiwemo la Makonda hayajapata madhara katika ajali hiyo.
Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo kujua chanzo cha ajali hiyo ambapo alijibu kuwa: "nilikuwa mbele ya msafara, siwezi kujua chanzo cha ajali, subiri tufanye uchunguzi nitakuambia.”
Msafara wa Makonda ulikuwa unatokea wilayani Songea kuelekea Dar ea Salaam baada ya mapema leo asubuhi kutangaza chama hicho kusitisha ziara katika mikoa ya Lindi na Mtwara iliyobaki kati ya mikoa 20.
Ziara hiyo imesitishwa ili CCM kuungana na wananchi wengine katika maombelezo ya kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyefariki dunia jana Jumamosi, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alipokuwa akipatiwa matibabu ya magonjwa ya kujikunja kwa utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
“Nilianza ziara yangu Januari 19, jana nikaingia Mkoa wa Ruvuma ikiwa ni mkoa wa 18 kati ya 20 niliyopanga kuitembelea, lakini kwa masikitiko makubwa tukatangaziwa msiba wa kuondokewa na mpendwa wetu, mzee Lowassa.
“Kutokana na msiba huo tulilazimika jana kufanya mkutano katika mazingira magumu, tusingeweza kuwaacha wananchi waondoke bila kusikiliza kero zao, lakini mwisho tumelazimika kuungana kwa vitendo kuombeleza msiba huu,” amesema Makonda.