MSD yasambaza dawa za Sh1 bilioni kwa siku

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai akizungumza na waandishi wa gazeti hili wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Loveness Bernard

Muktasari:

  • Ili kukabiliana na uhaba wa dawa katika vituo vya afya nchini, Bohari ya Dawa (MSD) imesema imekuwa ikisambaza tani 1,600 za dawa zenye thamani ya takribani Sh1 bilioni kila siku.


Dar es Salaam. Ili kukabiliana na uhaba wa dawa katika vituo vya afya nchini, Bohari ya Dawa (MSD) imesema imekuwa ikisambaza tani 1,600 za dawa zenye thamani ya takribani Sh1 bilioni kila siku.

Kutokana na usambazaji huo, mwaka wa fedha 2021/22 ilisambaza dawa za Sh324 bilioni.

Pamoja na hayo, pia imesema inashughulikia changamoto za ndani na nje zinazosababisha tatizo la ufinyu wa dawa, ikiwamo kuanza kujiendesha kwa mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Akizungumza na Mwananchi jana katika mahoajino maalumu jijini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai alisema kuna masuala yaliyokuwa yakichelewesha ufikishwaji wa dawa vituoni ambayo yamefanyiwa kazi, huku akiutaja mkakati wa matumizi ya Tehama.

“Kwa sasa usambazaji wetu ni asilimia 56, hii ni kwa upande wa zile dawa muhimu 290, ila mpaka Januari tunatarajia utafika asilimia 60 na utapanda mpaka asilimia 70 itakapofika Aprili,” alisema Tukai.

Kati ya vitu vinavyosababisha upungufu huo, Tukai alisema ni mikataba na wazabuni kwamba kati ya bidhaa za dawa 1,085 zinazohitajika, mikataba iliyokuwapo ilikuwa asilimia 36 tu, lakini juhudi zimefanyika na sasa imepanda mpaka asilimia 85.

Licha ya uchache wa mikataba hiyo, alisema baadhi ya wazabuni hawafikishi dawa hizo kwa wakati, lakini MSD inakijengea uwezo kitengo cha ‘compliance’ ili kuwabana wahusika watakaokiuka mikataba yao.

“Changamoto nyingine tunaagiza dawa lakini kwenye kupokea ni wazabuni wachache wanaofikisha dawa kwa wakati, wengi wanachukua muda mrefu, katika oda zinazoagizwa tunazozipokea kwa wakati ni asilimia 30, hii ni changamoto na ukiangalia kwa zile oda moja moja tumepokea asilimia 50 mpaka sasa,” alisema.

Alisema kwa sasa taasisi hiyo imekuwa ikitoa adhabu mbalimbali kwa mujibu wa mikataba.

Alipoulizwa kuhusu changamoto ya uwepo wa dawa zinazobaki pasipo kutumika huku nyingine zikionekana kuhitajika zaidi vituoni na kukosekana, Tukai alisema imekuwa ikisababishwa na maoteo (makadirio).

“Kuna changamoto kubwa katika maoteo ya dawa, nadhani kuna shida katika maeneo mengi, ikiwamo eneo la takwimu,” alisema.

Pamoja na hayo, Tukai alisema kuna mabadiliko yaliyofanyika na yanaendelea kufanyika ili kuhakikisha wanaondoa mianya yote ya rushwa na ubadhirifu ndani ya taasisi kwa kuweka mifumo mipya hasa katika manunuzi.

“Kwa sasa tunashirikiana na bodi ya wataalamu ya ununuzi na ugavi (PSPTB), Baraza la Famasia na Wizara ya Afya; tayari tumeandaa mfumo rasmi wa Tehama kuanzia zabuni, manunuzi na mchakato wote utafanyika kupitia mfumo wa Tehama,” alisema Tukai.

Akitoa mfano wa vitanda, alisema kwa sasa wanaangalia namna ya kununua bidhaa kutoka kwa wazalishaji wa ndani, ambapo alisema mahitaji ya sasa ni vitanda 3,600 na uwezo wa uzalishaji vitanda kwa viwanda vya ndani ni mdogo hivyo wanalazimika kuagiza nje.

“Tuna changamoto ya vitanda nchi nzima na ukiangalia uhitaji ni vitanda 3,600, MSD tumefanikiwa kuagiza vitanda 2,000 na kati ya hivyo vipo vilivyowasili na vingine 1,000 tunatarajia kupokea Februari mwakani,” alisema.

Licha ya changamoto zote, Tukai alisema MSD imekuwa ikisambaza dawa, vifaa na vifaa tiba vya takribani thamani ya Sh1 bilioni kila siku katika vituo vyote nchi nzima.

“Kwa siku tunasambaza dawa tani 1,600 na tunapowafikia watu asilimia 56 hapo ni sawasawa umewafikia watu milioni 30 na hapo tunaangalia namna ya kufikisha kwa haraka kwa kutumia magari tuliyonayo na hivi sasa MSD inafikisha dawa mpaka kwenye zahanati mpaka maeneo yasiyofikika,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu suala la usambazaji dawa nchi za SADC jukumu ambalo MSD ilikabidhiwa mwaka 2017, Tukai alisema mchakato huo umeanza upya na Februari mwaka 2023 wanatarajia kuwa na mkutano mkuu wa pamoja utakaofanyika hapa nchini.


Dawa kuharibika

Katika ripoti ya CAG iliyotolewa Machi mwaka huu, ilionyesha MSD ilibaki na shehena ya dawa za Sh7 bilioni zilizokuwa zimeharibika, hivyo kusababisha hasara.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Tukai alisema kuna changamoto kubwa ya mnyororo wa ugavi kuanzia katika uagizaji dawa, zinapofika nchini mpaka usambazaji.

“Kuna changamoto nyingi, mfano tumepima Uviko-19 lakini kwa sasa hatupimi, MSD tunavyo vipimo bado ‘rapid test’ zitabaki na kuharibika,” alisema.

Pia, alisema ikiwa kwa siku MSD inasambaza dawa za Sh1 bilioni, kuharibika kwa kiasi hicho cha dawa ni sawa na asilimia 2 ya dawa zote zinazopokewa, kiwango kinachokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO).