Msekwa: Asiyeupenda Muungano akajinyonge

Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa

Muktasari:

Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa amesema mtu asiyependa Muungano wa Tanzania akajinyonge.

Dodoma. Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa amesema mtu asiyependa Muungano wa Tanzania akajinyonge.

Msekwa ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 26, 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusu hatua mbalimbali ambazo viongozi wa Tanganyika na Zanzibar walipitia kabla ya Muungano.

Msekwa amesema Muungano wa Tanzania utadumu milele kuliko watu walivyodhani na kwamba hana shaka yoyote kuhusu hilo kwani anayaona mema.

"Muungano utadumu milele na milele,lakini asiyeupenda Muungano basi akajinyonge, tumepita kwenye mengi lakini mafanikio ni makubwa," amesema Msekwa.

Ameeleza historia ya waasisi wa Muungano ambao ni Hayati Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume akisema kulikuwa na ulazima kuungana kutokana na hofu iliyokuwa imetanda kwa wakati huo kuhusu Zanzibar.

Amesema usalama wa Zanzibar ulikuwa shakani kwa sababu ya hofu ya waliopinduliwa kwambe huenda wangerudi tena katika eneo lao.

Kwa upande wake Balozi, Dk Getrude Mogella amesema wanaoongoza Taifa ni watoto wadogo lakini wanapaswa kuheshimiwa kwa nafasi zao.

Dk Mogella amesema ni utamaduni wa kawaida wazee wakifikia umri fulani kuwapisha vijana kushika usukani wa kiuongozi hivyo lazima kukubaliana na hilo.