Prime
Chunga haya unapotafuta mwenza wa maisha
Muktasari:
- Watu wengi husema kuwa ni rahisi kukosea kujenga nyumba kuliko kukosea kuchagua mwenza wa maisha.
Dar es Salaam. Kumtafuta mwenza wa maisha ni moja ya maamuzi nyeti na ya muda mrefu katika maisha ya binadamu. Si jambo la papara wala la kufuata hisia za muda mfupi, bali linahitaji tafakuri ya kina, maandalizi na uelewa mpana wa maisha.
Makosa yanayofanyika katika hatua hii huweza kuacha madhara ya muda mrefu, si tu kwa wahusika wawili bali hata kwa familia na jamii kwa ujumla. Ndiyo maana watu wengi husema kuwa ni rahisi kukosea kujenga nyumba kuliko kukosea kuchagua mwenza wa maisha. Hivyo basi, ni muhimu kuzingatia mambo kadhaa kabla ya kufanya uamuzi huu mkubwa.
Elimu ni muhimu
Elimu ni nyenzo muhimu katika maisha ya kila siku, hasa katika kuelewa dunia na kujenga msingi wa kiuchumi.
Hata hivyo, katika suala la kuchagua mwenza wa maisha, elimu haipaswi kuwa kigezo cha kwanza au cha pekee.
Baadhi ya watu wamekuwa wakifanya makosa ya kuchagua wenza kwa kuangalia kiwango cha elimu pekee, wakidhani kwamba cheti au shahada ndiyo dhamana ya ndoa yenye mafanikio.
Ukweli ni kwamba ndoa haijengwi na elimu pekee bali na upendo, uvumilivu, maadili na maelewano. Kuna watu wenye elimu ya juu lakini hawana uthabiti katika uhusiano, na wengine wenye elimu ya kawaida lakini ni waaminifu, wenye heshima na wanaojitambua.
Ni muhimu kutambua kwamba watu wanaoweza kukusukuma kufanya uamuzi wa maisha kwa misingi ya “watu watasemaje” mara nyingi hawatakuwapo wakati changamoto halisi za ndoa zitakapotokea. Hivyo, chagua kwa kuzingatia tabia na maadili, si cheti pekee.
Kabila au asili isiwe kigezo
Katika jamii nyingi, bado kuna mtazamo wa kuchagua mwenza kwa kuzingatia kabila au asili. Ingawa utamaduni una nafasi yake muhimu katika maisha ya binadamu, si sahihi kuufanya kuwa kizuizi cha kupata mwenza sahihi. Upendo na maelewano havijifungi katika mipaka ya kikabila.
Kuna watu ambao huweka msisitizo mkubwa kwamba lazima waoe au waolewe kutoka katika makabila yao pekee, hali ambayo wakati mwingine huwanyima nafasi ya kukutana na watu sahihi zaidi. Ukweli ni kwamba, si kila mtu wa kabila lako atafaa na maono yako ya maisha, na si kila wa kabila jingine atakuwa kinyume nawe.
Kilicho muhimu zaidi ni tabia, maadili, malengo ya maisha na uwezo wa kuishi kwa amani na mwenzi wako.
Ndoa bora ni ile inayojengwa na watu wawili wanaoelewana na kuheshimiana, bila kujali tofauti za kikabila. Hivyo, badala ya kuangalia asili, ni vyema kuzingatia utu wa mtu na mwelekeo wa maisha yake.
Ushauri ni muhimu
Wazazi, walezi na marafiki wana nafasi kubwa katika kutoa ushauri kuhusu uchaguzi wa mwenza wa maisha. Ushauri wao unaweza kuwa wa manufaa kwa kuwa wana uzoefu na wanaweza kuona mambo ambayo wewe huenda huyoni. Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya ushauri na shinikizo.
Baadhi ya watu huingia katika ndoa si kwa hiari yao, bali kwa kushinikizwa na familia au jamii. Wengine huchagua wenza kwa kuangalia hadhi ya familia ya mchumba badala ya tabia ya mtu mwenyewe. Hili ni kosa ambalo mara nyingi huzaa migogoro ya muda mrefu katika ndoa.
Ni muhimu kusikiliza ushauri, lakini uamuzi wa mwisho uwe wako. Usiruhusu shinikizo la jamii au matarajio ya watu wengine yakufanye uingie katika uhusiano usio sahihi. Maisha ya ndoa ni ya watu wawili, si ya familia au jamii pana.
Kwa ujumla, kuchagua mwenza wa maisha ni uamuzi unaohitaji hekima, uvumilivu na tafakari ya kina.
Elimu, kabila na ushauri wa familia ni mambo muhimu, lakini havipaswi kuwa msingi pekee wa uamuzi. Kilicho cha msingi zaidi ni tabia, maadili, upendo wa kweli na maelewano kati ya wahusika.
Ni vyema kila mmoja akajipa muda wa kutosha kumtambua mwenzia wake kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia katika ndoa.
Maisha ya baadaye yanategemea sana uamuzi tunofanya leo. Hivyo, chagua kwa busara, tafakari kwa kina, na epuka kufanya uamuzi wa haraka utakaokuumiza baadaye.