Mshahara mpya wazusha gumzo

Samia asema nyongeza ya mshahara ipo

What you need to know:

Wakati Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) likieleza kuridhika na kauli ya matumaini ya Serikali kuhusu nyongeza ya mishahara, baadhi ya wadau wakiwemo wanasiasa, wachumi na wanaharakati wameibua hoja tofauti wakihoji sababu za mchakato huo kuchelewa na kiwango kutowekwa wazi.

Dar es Salaam. Wakati Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) likieleza kuridhika na kauli ya matumaini ya Serikali kuhusu nyongeza ya mishahara, baadhi ya wadau wakiwemo wanasiasa, wachumi na wanaharakati wameibua hoja tofauti wakihoji sababu za mchakato huo kuchelewa na kiwango kutowekwa wazi.

Wadau hao wamesema kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya “kuendelea kwa mahesabu” inaashiria kurefusha mchakato huo bila sababu huku wafanyakazi waliendelea kusubiria.

Katika hotuba wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani juzi, Rais Samia alisema mahesabu yanaendelea ili kujua nyongeza itakuwaje.

“Ulezi wa mama unaendelea. Lile jambo letu lipo, sio kwa kiwango kilichosemwa na Tucta (kima cha chini Sh1,010,000) kwa sababu hali ya uchumi wa nchi yetu na uchumi wa dunia si nzuri.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Rais wa Tucta Tumaini Nyamhokya alisema wao kama wawakilishi wa wafanyakazi wanafahamu kiwango cha mishahara kitakachoongezwa, lakini hawawezi kukibainisha bila idhini ya mamlaka.

Alifafanua kuwa mchakato ulifanyika baada ya majadiliano kati ya mamlaka na wawakilishi wa wafanyakazi, hivyo nyongeza hiyo imezingatiwa hata katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

“Tunajua kinachoendelea. Tunajua kiasi gani kimeongezwa kwa sababu tulikubaliana na mamlaka kwenda hivyo, lakini Rais hakutaja kwa sababu maalumu, nami siwezi kutaja,” alisema.


Maoni mbadala

Kinyume na mtazamo huo wa Tucta, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema: “Rais mwaka jana alisema ‘mimi mama yenu mwakani nitaongeza mishahara.’ Sasa mwaka mzima wanakokotoa nini hadi leo asitoe kauli ya moja kwa moja?”

Mbatia alibainisha kuwa mambo hayo huwakosesha wafanyakazi tumaini na kusababisha migogoro.

“Ili twende sawa katika mambo mbalimbali tunahitaji utulivu wa fikra na kufanikisha hilo, tukubali au tukatae tunahitaji muafaka wa kitaifa. Muafaka utatuwezesha kukaa pamoja kuaminiana na kuzungumza tunataka nini,” alisema Mbatia.

Msimamo wa Mbatia hauna tofautiana na wa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Addo Shaibu aliyesema chama hicho hakikuridhishwa na kauli ya Rais Samia kuhusu kuendelea kushughulikiwa kwa nyongeza ya mishahara.

Addo alisema kauli ya Rais inarefusha mchakato huo na kimsingi inaendelea kuwasababishia wafanyakazi maumivu ya maisha.

“Tumeshazoea ulimwenguni katika maadhimisho ya Mei mosi ndipo mwajiri anatoa tumaini na mwelekeo wa mwaka ujao kwa mfanyakazi wake,” alisema.

Kwa upande wake Chadema ilikwenda mbali zaidi ikilinganisha na hali ya hapa nchini na ilivyo katika nchi nyingine jirani.

Makamu mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu alieleza kushangaa Rais Samia kushindwa kutamka kuongeza mishahara kama alivyoahidi mwaka jana.

“Tujiulize, Kenya iliyoweka watu ‘lockdown’ imewezaje kuongeza asilimia 12 ya mshahara ilhali Tanzania ambao hakuna mtu aliyefungiwa ndani lakini ikashindwa kuongeza mshahara?” Hata wafanyakazi wanashindwa kutetea maslahi yao wanaishia kujipendekeza na kubaki ombaomba, ili hali hii iweze kufikia ukomo lazima tupate Katiba mpya ambayo itasimamia maslahi ya Watanzania,” alisema Lissu alipotoa maoni yake wakati wa kongamano la Vijana wa Chadema lililofanyika kwa njia ya mtandao.

Lakini, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kinachojitokeza ni makosa wafanyakazi kukaa miaka saba bila ya nyongeza ya mishahara ilhali gharama za maisha zinaongezeka.

“Huko nyuma ilikuwa kila mwaka mishahara inaongezeka, makosa yalifanyika awamu iliyopita kuwaacha wafanyakazi miaka mingi bila nyongeza ya mishahara kunadhoofisha ari na tija katika kazi zao,” alisema.

Alishauri nia iliyoonyeshwa na Rais Samia kuhusu kuongeza mishahara iwe endelevu kila mwaka na watumishi walipwe kuendana na uhalisia wa gharama za maisha.

Akiunga mkono hilo, Anna Henga, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alisema pamoja na nyongeza ya mishahara, nyongeza hiyo inapaswa kuendana na mfumuko wa bei na Serikali haina budi kuongeza mishahara ya watumishi kila mwaka ili kutekeleza haki yao hiyo.

“Nyongeza ni wajibu wa Serikali kila mwaka, lakini mimi si muumini wa kutangaza, waongeze mishahara wapitishe waraka kimya kimya, watu wawe na uchumi endelevu. Ukitangaza kuna watu watapandisha bei za bidhaa,” alionya.

Wakati huohuo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewapongeza wafanyakazi kwa tamko lao la kumuunga mkono Rais Samia juu ya nyongeza ya mishahara.

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema jana kuwa: “Katibu Mkuu wa Tucta amesema walikutana na Rais siku moja kabla ya sherehe za Mei mosi na kukubaliana juu ya ajenda hiyo (nyongeza ya mishahara).

“Na kwamba Rais Samia aliwahakikishia kuwa Serikali itapiga mahesabu na nyongeza hiyo itapatikana katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai 2022,” alisema Shaka.

Alisema uamuzi wa Rais Samia kukubali wafanyakazi waliofukuzwa baada ya kukutwa na vyeti bandia kulipwa stahiki zao, unapaswa kuungwa mkono kwani wengi waliathirika.

“Rais Samia anasimamia maslahi mapana ya wafanyakazi nchini, alichokifanya sio porojo ama utashi wake bali ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini,” alisema Shaka.