Mshitakiwa akana uraia wa DR Congo

Muktasari:
- Mshtakiwa Pacific Mwenas anayekabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuishi nchini bila ya kibali, amekanusha kuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwamba hajawahi kuishi nchini humo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kusikiliza mashahidi watatu katika kesi inayomkabili Pacific Mwenas anayedaiwa kuwa raia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo akikabiliwa na mashtaka mawili ya kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria.
Wakili wa Serikali, Shija Sitta amedai hayo leo Septemba 27, 2023 wakati akimsomewa hoja za awali mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, akisema Septemba 12 mwaka huu katika kituo cha pamoja, mshtakiwa huyo alikutwa akiwa hana kibali cha kuishi nchini.
Amedai kuwa mshitakiwa huyo aliwadanganya maofisa wa uhamiaji kuhusu uraia wake ni wa Tanzania wakati akijua sio kweli.
Wakili Sitta amedai Septemba 13, 2023 mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yake, ambapo amekiri kuishi nchini, lakini akakana kuwa yeye si raia wa Congo DR wala hajawahi kuishi katika nchi hiyo.
Amesema kwamba baba yake ni Mtanzania ila mama yake ndio raia wa Congo DR.
Wakili Sitta alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwa upande wa Jamhuri watakuwa na mashahidi watatu wakati wa usikilizwaji.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 11, 2023. mshtakiwa alipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana likiwemo kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh1 milioni.